Mgonjwa mahututi afa kwa ajali akihamishiwa hospitali rufani


Mgonjwa mahututi aliyekuwa akihamishiwa hospitali ya Rufani Bombo, mkoani Tanga amefariki dunia baada ya gari ya kubebea wagonjwa (ambulance) kugongana uso kwa uso na lori la mizigo katika eneo la Saruji, jijini humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema katika ajali hiyo watu wengine wanne wamejeruhiwa.

Ajali imetokea usiku wa saa sita kuamkia leo, Machi Mosi, 2026, gari ya wagonjwa lilitokea wilayani Korogwe na gari la mizigo likitoka jijini Arusha.

Kamanda amesema gari la wagonjwa ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, lenye namba STM 7202 na lilikuwa likiendeshwa na Alphonce Alfan, mkazi wa Korogwe.

Gari la mizigo aina ya Scania lenye namba T 628 DSG, na Tela namba T 637 DSG, likiendeshwa na John Philipo, mkazi wa Arusha.

Amemtaja aliyepoteza maisha kuwa ni Zaharia Mode (41), mkazi wa Kijiji cha Goha wilayani Korogwe, ambaye alikuwa akihamishiwa hospitalini huko, kwa matibabu zaidi,ndugu watatu pamoja na muuguzi nao ni majeruhi.

Aidha amewataja majeruhi kuwa ni Zainabu Mode, Selemani Mode na Naiman Mode ambao ni ndugu wa marehemu pamoja na Habibu Hatibu ambaye ni muuguzi na wote wamekumbizwa Hospitali ya Rufani Bombo, kwa matibabu.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa gari la wagonjwa, ambaye alikuwa kwenye mwendo kasi, ndipo gari lilipomshinda na kuhama upande wa pili, aligongana uso kwa uso na lori.

Related Posts