
Kiongozi wa Kanisa la Arise and Shine, Mchungaji Apostle Boniface Mwamposa.
DAR ES SALAAM: Kiongozi wa Kanisa la Arise and Shine, Mchungaji Apostle Boniface Mwamposa, amesema alimkataa aliyekuwa bilionea wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, kuhudhuria mkesha uliofanyika hivi karibuni nchini Tanzania.
Mwamposa amesema Chivayo alipiga simu akieleza nia yake ya kusafiri kutoka Zimbabwe na kuhudhuria mkesha huo, lakini aliamua kutomruhusu kutokana na hofu ya tukio hilo kutafsiriwa kisiasa.Amesema Chivayo anajulikana kwa kutoa fedha kwa baadhi ya wachungaji, hivyo uwepo wake kwenye mkesha ungeweza kuwafanya baadhi ya watu kuhusisha shughuli za kanisa na fedha kutoka kwake.
“Walipiga simu anataka kuja kwenye mkesha kutoka Zimbabwe, nikasema hapana. Ni kweli anatoa kwa wachungaji wengi, akija wapo watu watuchukulia kisiasa. Pili, watu watadhani vitu vyote tunavyovifanya hivi huwa tunachukua hela kwake,” amesema Mwamposa.Mwamposa amesisitiza kuwa mafanikio ya shughuli wanazofanya yanatokana na Mungu na si msaada wa bilionea huyo.“Nataka watu wajue ni Mungu anatufanikisha,” amesema.Chivayo ni mfanyabiashara kutoka Zimbabwe ambaye amekuwa akijulikana pia kwa kutoa misaada na michango kwa viongozi mbalimbali wa dini nchini humo.
Global publishers
