
Mwanafunzi wa darasa la nne afariki kwa kujinyonga Morogoro
Mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mwenge, Manispaa ya Morogoro, Oscar James Sagina (9), amefariki dunia katika mazingira yanayodaiwa kuwa ya kujinyonga, siku chache kabla ya kufanya mtihani wake.
Oscar amefariki Oktoba 2, 2026, nyumbani kwao katika Mtaa wa Tangi la Maji, Kata ya Kingolwira, huku Jeshi la Polisi likiendelea kuchunguza mazingira ya tukio hilo.
Baba mdogo wa marehemu, Masaga James Sagina, amesema Oscar alikuwa akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake wawili, na familia bado haijabaini sababu iliyosababisha kifo hicho.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Tangi la Maji, Mohamed Abdalah, amesema tukio hilo ni la pili katika eneo hilo kumhusisha mwanafunzi wa darasa la nne aliyekuwa akitarajiwa kufanya mtihani, akiwataka wazazi kuongeza mawasiliano na watoto wao ili kufahamu changamoto wanazopitia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amethibitisha kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza tukio hilo.
Katika taarifa ya maandishi, Kantimbo amesema suala la maandalizi ya mtihani lilitajwa katika taarifa za awali kuhusu tukio hilo, ingawa uchunguzi unaendelea kubaini mazingira na sababu za kifo hicho.
