
Mfanyabiashara na Mkazi wa Butimba jijini Mwanza, Elizabeth Chacha Mugusuhi (30), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, leo Agosti 6, 2026 na kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili katika Kesi ya Jinai Namba 1012/2026.
Kwa mujibu wa hati ya Mashtaka, Mshtakiwa alitenda makosa hayo Julai 25, 2026 katika eneo la Kituo cha Polisi Nyegezi, ambapo kosa la kwanza ni kutoa taarifa za uongo kwa Watumishi wa umma kinyume na kifungu cha 122(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2023. Kosa la pili ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 302 cha sheria hiyo hiyo.
Akisoma hati ya Mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni, Mhe. John Mgonya, Mwendesha Mashtaka Sajenti Doroth Mauma amesema Mshtakiwa alitenda makosa hayo akijua wazi kuwa ni kinyume na sheria.
“Wewe Elizabeth Chacha Mugusuhi, mnamo Julai 25, 2026 majira ya saa 8:00 usiku katika maeneo ya Kituo cha Polisi Nyegezi, ulitoa taarifa za uongo kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi kuwa umetekwa na watu wasiojulikana huku ukijua kuwa ni kosa kisheria. Pia, siku hiyo hiyo majira ya saa 8:00 usiku, ulijipatia kiasi cha Sh 800,000/= kwa njia ya udanganyifu ulizoomba utumiwe kwa madai kuwa umetekwa,” alisema Sajenti Doroth.
Hata hivyo, Mshtakiwa baada ya kusomewa Mashtaka mawili yanayomkabili, amekiri kutenda makosa hayo na kuiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na ana watoto wadogo wanaomtegemea.
Akitoa hukumu katika kesi hiyo, Mhe. Mgonya amesema kwa kuwa ni makosa yake ya kwanza na hakuisumbua Mahakama kwa kukiri kosa, Mahakama imeona impatie adhabu itakayokuwa fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
“Mahakama inatoa adhabu ya kifungo cha nje cha miezi sita kwa Mshtakiwa chini ya Kifungu cha 2(1)(a) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 Nyongeza ya III Marejeo ya mwaka 2023, pamoja na kufanya kazi za jamii kwa kipindi chote cha kifungo hicho. Iwapo mshtakiwa atakiuka masharti haya, kifungo hiki kitabadilika na kuwa cha ndani,” amesema Hakimu Mgonya.
