Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa kwa siku tano kuanzia Jumapili, tarehe 25 Mei hadi Alhamisi, tarehe 29 Mei 2025. Katika taarifa hiyo, TMA imeeleza kuwepo kwa upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa pamoja na mawimbi makubwa yanayofikia hadi mita 2 katika maeneo yote ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi. Maeneo yanayoathirika ni pamoja na mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Upepo na mawimbi hayo yanatarajiwa kuwa na athari za wastani, ambapo shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakuwa hatarini. Shughuli hizi ni pamoja na uvuvi, usafirishaji baharini na biashara zinazotegemea usafiri wa majini. TMA imetoa wito kwa wananchi wote, hasa wale wanaoishi au kufanya shughuli katika ukanda wa pwani, kuchukua tahadhari kubwa na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Kwa mujibu wa ramani zilizowekwa katika taarifa hiyo, maeneo yaliyoathirika yamechorwa kwa rangi ya njano, ikiwa ni ishara ya angalizo, na kuonyesha wazi athari zinazotarajiwa. Katika kila siku ya utabiri, kuanzia Jumapili hadi Alhamisi, hali hiyo ya upepo mkali na mawimbi makubwa inaendelea kuonekana katika maeneo hayo.
Wananchi wanahimizwa kufuatilia taarifa rasmi kutoka TMA na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya usalama wao, mali zao na shughuli zao za kiuchumi. Kauli mbiu inayosisitizwa na TMA kwa siku hizi tano ni: “Zingatieni na Jiandaeni.”

