Nature

Tuhuma za ‘Umeme Kuzimwa kwa Makusudi’ TANESCO Yatoa Tamko

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni zikilihusisha na matukio ya kihalifu huku likielezea kusikitishwa na taarifa hizo ambazo limedai si za kweli, na hazihusiani kwa namna yoyote na majukumu ya Shirika ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa huduma ya umeme nchini.

Taarifa ya TANESCO iliyotolewa Desemba 1, 2025 imeeleza kuwa kwamba kukatika kwa umeme kunaweza kusababishwa na sababu mbalimbali za kiufundi, ikiwemo hitilafu za dharura kwenye miundombinu au matengenezo yaliyopangwa ili kuboresha upatikanaji wa huduma. Mambo haya yote ni ya kitaalamu, yanaratibiwa kwa mujibu wa taratibu, na hayana uhusiano wowote na vitendo vya kihalifu.

Taarifa ya TANESCO masaa kadhaa baada ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dkt. Charles Hugo Kitima kusikika akitoa kauli kwamba watekaji walishirikiana na TANESCO kuzima umeme ili kumdhuru.

“Skenario ya wasiojulikana hazijaanza hapa. Kwanza nilikuwa sijui, lakini baadaye nikajua kupitia waliokuja kunivamia, kwanza TANESCO walizima umeme ili niuawe. Nikaona hizi mbinu ni kama mkakati umepangwa.” — alinukuliwa Dkt. Kitima katika mahojiano na vyombo vya habari mnamo Desemba 1, 2025.

Aidha TANESCO imetoa wito kwa wananchi kuepuka kutoa au kusambaza taarifa zisizothibitishwa zinazoweza kupotosha umma na kuathiri taswira ya Shirika hilo huku lkisisitiza kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kitaalamu kwa weledi na uadilifu, na kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika kwa wateja wake kote nchini.

Related Posts