Umeme wakatika Muhimbili kwa saa 15, wagonjwa wahaha
Dar es Salaam. Wagonjwa wanaopokea huduma ya kuchuja damu ‘dialysis’ katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, MNH wamelalamikia jengo la watoto hospitalini hapo kukosa umeme kwa saa 15 mfululizo, hali iliyoathiri matibabu yao.
Matibabu ya dialysis kawaida hujumuisha kutumia mashine kuchukua kazi ya figo kuchuja sumu, taka na maji kupita kiasi kutoka mwilini. Tiba hii huhitajika kwa wagonjwa ambao figo zao hazifanyi kazi vizuri au zilizofeli.
Akijibu suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MNH, Aminiel Aligaesha amekiri kutokea kwa hitilafu hiyo na kueleza hatua zinazochukuliwa kwa sasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi leo Jumatatu, Mei 26, 2025 wagonjwa hao wamesema umeme huo ulikatika jana saa tatu usiku, kabla ya kuwashwa jenereta ambalo nalo liliharibika baada ya muda mfupi.
Wagonjwa hao ambao hawakutaka kutajwa majina yao kwa sababu za kiusalama, wamesema hali hiyo imesababisha baadhi yao kuanza kupata athari hasi kwa kuvimba miguu, matumbo na kutapika.
“Jengo lote umeme ulikatika jana usiku saa tatu, jenereta likawashwa nalo likazima, wanasema ni mbovu, wameleta mafundi wanatengeneza lakini watu wa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) hawajafika mpaka sasa hatuna matibabu, hata wagonjwa waliokuwa ICU wamehamishiwa kwenye majengo mengine,” amesema mmoja wa wagonjwa hao.
Amesema hakuna matibabu yanayoendelea kwa sasa, “Wagonjwa wa figo tuko nje tumekaa tu, viongozi wanapita wanatuambia kama unajisikia hauko vibaya sana unaweza kwenda kupumzika nyumbani.”
Mgonjwa mwingine amesema eneo lote la jengo watoto hakuna huduma inayoendelea kwa sasa na yeye amefika toka jana hajafanikiwa kupata huduma.
“Watu wamezidiwa, wengine wapo hoi kabisa na hatujui chochote kinachoendelea, ratiba yangu ilibidi niwe nimepata matibabu mzunguko wa saa 4 usiku, lakini mpaka sasa nimenasa hapa sijapata matibabu.
“Kiukweli kadri masaa yanavyosogea wagonjwa wanaanza kuchoka, sisi figo zote zimekufa tunategemea hizi mashine, wengine wameshazidiwa matumbo yamejaa, miguu imevimba, wengine wanatapika, watoto huko juu wako hoi wamehamishwa wodi wengine wamepelekwa wodi zingine,” amesema.
Mkazi wa Tegeta ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema mtoto wake amelazwa katika moja ya wodi na wamepambana na giza usiku kutokana na kukosekana kwa umeme.
“Wenzetu wenye hali mbaya watoto wao wamehamishwa, wamepelekwa wodi zingine hasa wale ambao walikuwa wanatumia oksijeni na waliokuwa ICU, sasa tunapambana na joto maana hakuna umeme usiporudi tutalala tena gizani,” amesema mama huyo.
Muhimbili yachukua hatua
Aminiel amesema katizo la umeme katika jengo hilo limetokea jana usiku, “Usiku wa kuamkia leo Mei 26, 2025 saa tano usiku, kulijitokeza changamoto ya umeme katika jengo la watoto baada ya njia mbili za umeme kutoka na kusababisha kuwepo na hitilafu kwenye transfoma na kuathiri pia jenereta ya dharura.”
Amesema kilichotokea jengo hilo lina ‘phase’ tatu za umeme, mbili zilitoka ikabaki moja ambayo baadaye nayo ilitoka na kusababisha kukosekana kwa umeme katika jengo la watoto (NPC).
Amesema waliishirikisha Tanesco ambao nao walifika kwa wakati wakajaribu kuanza kutafuta hitilafu ni nini walifanikiwa kurudisha phase mbili zilizokuwa zimekatika, katika mchakato huo, kulitokea hitilafu kwenye transfoma ambayo ilisababisha madhara hadi kwenye jenereta ya dharura na kuunguza vifaa viwili muhimu, relay na CM (kadi ambayo hufanya kazi kama ubongo wa jenereta).
“Kwa hiyo tunachokifanya sasa toka jana saa sita usiku wa kuamkia leo Tanesco wako Muhimbili hawajalala na mafundi, pia tumemwita Delta ambaye ni mtoa huduma wa jenereta hili naye hajalala wote wako hapa, wanajaribu kuangalia tatizo ni nini kwa pamoja.”
Aminiel amesema kwa wananchi wanaopata huduma katika jengo hilo, wale ambao huduma zao zinategemea umeme kwa kiasi kikubwa wamehamishiwa kwenye wodi zingine.
“Tuna wagonjwa wanaohitaji huduma za ICU, tunayo ya watoto jengo hilo ambao tumewasambaza katika ICU zingine ili waendelee kupata huduma. Kulikuwa na watoto wa maeneo mengine, wengine wako kitengo cha dharura sehemu ya watoto na wengine tumewapeleka jengo la wazazi,” amesema.
Kuhusu hatma ya wagonjwa wa dialysis, Aminiel amesema tayari hospitali imechukua hatua za haraka kuwasiliana na hospitali zingine za karibu, “Tunawasiliana na hospitali jirani ili waendelee kusafishwa figo, sisi tuna wagonjwa wengi kwa siku. Jitihada ziko palepale kuhakikisha tunarejesha umeme.”
Meneja wa Tanesco mkoa wa Ilala, Regina Mvungi amesema mafundi wanaendelea na matengenezo tangu jana usiku, “Tulipeleka mafundi tangu jana usiku, mpaka sasa bado wanaendelea na matengenezo kama kungekuwa na changamoto kubwa zaidi ningetaarifiwa, nadhani muda si mrefu watamalizia.”