
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia raia wanne wa China wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la utekaji wa wafanyabiashara wawili wenzao, ambao walikuwa wametekwa na baadaye kuokolewa katika oparesheni maalum ya polisi iliyofanyika Mei 16, 2026.
Wafanyabiashara hao walitekwa wakiwa katika majengo pacha ya PSSSF jijini Dar es Salaam kabla ya kupatikana wakiwa salama kupitia juhudi za kiintelijensia na operesheni ya vyombo vya usalama.
Akitoa taarifa hiyo leo Jumatatu, Mei 25, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema tukio hilo lilitokea Mei 14, 2026 majira ya saa 7:30 usiku baada ya polisi kupokea taarifa za kutekwa kwa raia hao, Weiyi Chen (64) na Liang Xiolo (44), ambao ni wafanyabiashara.
Ameeleza kuwa watu hao walivamiwa na kundi la watu saba na kisha kusafirishwa kwenda eneo lisilofahamika, ambapo baadaye watekaji walituma vitisho kwa familia za waathirika wakidai fidia ya dola milioni 20 za Marekani (takribani Sh52.2 bilioni) ili kuwaachia huru.
Kamanda Muliro ameongeza kuwa uchunguzi wa awali umebaini baadhi ya magari yaliyotumika katika tukio hilo, yakiwemo Toyota Alphard lenye namba T305 DRA ambazo zilionekana kuwa si halali pamoja na Toyota Harrier lenye namba T188 DHT.
