
Watengenezaji na Wasambazaji Clip za Jinai Wakamatwe
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kulichafua Jeshi hilo pamoja na Serikali kwa ujumla, kwa lengo la kusababisha uchochezi na kuvuruga amani na utulivu nchini.
Katambi amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia majukwaa hayo kusambaza taarifa na ujumbe unaolenga kulidhalilisha Jeshi la Polisi na taasisi za Serikali, hali inayoweza kujenga chuki miongoni mwa wananchi na kuathiri imani ya umma kwa vyombo vya dola.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halipaswi kuyafumbia macho matendo hayo, bali linapaswa kuendelea kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria kwa kuchukua hatua dhidi ya wote wanaobainika kujihusisha na vitendo vya uchochezi na matumizi mabaya ya majukwaa ya mawasiliano.
Ametoa maagizo hayo leo wakati akizungumza katika hafla ya kufunga Mkutano wa Mwaka 2026 wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi iliofanyika mjini katika Shule ya Polisi Tanzania Moshi, mkoani Kilimanjaro.
