Wizara ya Afya yapiga marufuku matumizi ya ‘risasi’ kuziba meno


Wizara ya Afya yapiga marufuku matumizi ya ‘risasi’ kuziba meno
Wizara ya Afya, imeagiza hospitali zote za umma na binafsi pamoja na kliniki binafsi za meno nchini, kusitisha matumizi ya ‘dental amalgam’, maarufu kama risasi katika kuziba meno kutokana na madhara kiafya na kimazingira.

Badala yake, vituo vya afya sasa vinatakiwa kutumia dawa mpya ya kujaza meno inayojulikana kama Cention N, ambayo haina kemikali ya zebaki (mercury).

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo maalumu kwa wataalamu wa meno na maofisa wa afya ya meno kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, amesema hatua hiyo inalenga kulinda afya za watanzania.

Dk. Nzobo amefafanua kuwa ‘dental amalgam’ ina takribani asilimia 50 ya zebaki, kemikali ambayo inaweza kuingia mwilini kupitia mvuke unaotolewa baada ya meno kujazwa.

Amesema mvuke huo huingia kwenye damu na kusambaa katika viungo mbalimbali vya mwili, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kuharibika kwa figo, matatizo ya mfumo wa fahamu na ubongo, pamoja na kuathiri ukuaji wa watoto waliopo tumboni na wadogo.

Aidha, amesema matumizi ya ‘amalgam’ yamekuwa yakiongeza hatari kila mara mtu anapotafuna chakula au kupiga mswaki.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Minamata kuhusu matumizi ya zebaki, ulioanzishwa chini ya Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2017.

Dk. Nzobo amesema Tanzania ilisimamisha rasmi uingizaji na matumizi ya ‘dental amalgam’ tangu mwaka 2022 na imekuwa ikitafuta mbadala salama, imara na wenye ufanisi zaidi

Related Posts