Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia watu wanne wanaodaiwa kuhusika katika wizi wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) la Hospitali ya Manispaa ya Musoma, lililoibiwa tarehe 25 Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara SACP Pius Lutumo, gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili STM 7830 lilipatikana likiwa tayari limeanza kufanyiwa marekebisho ili kubadilishwa kutoka matumizi ya dharura na kuwa gari la kibiashara kwa kubeba watalii.
Kwq mujibu wa taarifa hiyo watuhumiwa waliokamatwa ni Goodluck Steven Chacha (26) mkazi wa Tarime mjini, Karume Kimwel (26) mkazi wa Arusha, Saidi Hussein Ramadhani (39) mkazi wa Engosengiu, Arusha na Elias Joachim Lyimo (53), mkazi wa Arusha.
Aidha Polisi wamesema uchunguzi wa kina unaendelea kubaini mtandao mpana zaidi unaoweza kuhusika katika tukio hilo, huku watuhumiwa wakitarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya taratibu kukamilika.
