Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga umepanga kukipa kikosi chao nusu ya fedha ambazo timu hiyo itapata kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa watafanikiwa kufanya hivyo mwishoni mwa wiki hii.
Kila timu inayofuzu robo fainali ya mashindano hayo, inavuna kiasi cha Dola 900,000 (Sh2.3 bilioni) na Yanga imepanga kuwapa wachezaji na maofisa wake wa benchi la ufundi, nusu ya fedha hiyo, kiasi cha Dola 450,000 (Sh1.2 bilioni) ikiwa itafanikiwa kupenya.
Ili ifuzu robo fainali, Yanga inahitajika kuibuka na ushindi wa tofauti ya mabao mawili au zaidi katika mchezo wake wa mwisho nyumbani wa hatua ya makundi dhidi ya JS Kabylie kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 1:00 usiku na kuombea FAR Rabat ipoteze dhidi ya Al Ahly ili yenyewe ifuzu robo fainali.
Nyota mpya wa Yanga, Allan Okello wakati akijaribu kumtoka mchezaji wa AS FAR katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga ilifungwa bao 1-0 Februari 8, 2026. Picha na Mtandao
“Tumeahidi kwamba wachezaji watachukua nusu ya fedha ambazo CAF watatupatia endapo tutafuzu robo fainali.
“Tunafahamu kuwa kufuzu kwetu hakutategemea matokeo yetu pekee, bali pia matokeo ya mchezo kati ya Al Ahly na ASFAR,” amesema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
Maandalizi ya mchezo huo muhimu tayari yako katika hatua za mwisho. Baada ya safari ngumu ya Morocco, wachezaji walipewa muda wa kupumzika kabla ya kurejea mazoezini.
“Baada ya safari ndefu, wachezaji walipumzika kwanza. Mazoezi yalianza tena juzi tulipoanza maandalizi ya mwisho ya mchezo,” amenukuliwa kiongozi huyo.
Kiungo mshambuliaji raia wa Gambia, Buba Jammeh akiwa anasalimiana na wachezaji wenzake baada ya kufika kwa mara ya kwanza mazoezini Yanga. Picha na Yanga
Kuna habari njema kwa kikosi cha Yanga, baada ya kiungo mshambuliaji raia wa Gambia, Buba Jammeh, kurejea kikamilifu mazoezini kuelekea pambano hilo. Jammeh alikuwa anatarajiwa kujiunga na timu Morocco lakini alilazimika kurejea Gambia baada ya pasipoti yake kuisha muda wake wa matumizi.
“Buba amerudi na amejiunga na mazoezi. Uwepo wake unaipa benchi la ufundi chaguo zaidi za kushambulia tunapopambana kusaka mabao,” kimethibitisha chanzo hicho.
