Mwanamitindo wa TikTok afariki kwa kula sumu Akiwa Online

UFILIPINO : Mwanamitandao maarufu wa masuala ya vyakula nchini Ufilipino, Emma Amit mwenye miaka 51, amefariki dunia baada ya kula kaa mwenye sumu anayejulikana kama ‘devil crab’.
Mwanamtandao huyo alikula kaa huyo mwenye sumu akiwa anaandaa maudhui ya mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa ya tukio hilo lilitokea Februari katika makazi yake ya pwani mkoani Palawan, muda mfupi baada ya kurekodi video akila samakigamba hao aliowakusanya katika msitu wa mikoko karibu na Puerto Princesa.

Inaelezwa kuwa Amit akiwa na marafiki zake walikusanya kaa hao kisha kuwapika kwa tui la nazi kwa ajili ya video yake. Alionekana kuonja chakula hicho mbele ya kamera, lakini muda mfupi baadaye hali yake ilibadilika ghafla.

Mashuhuda wanasema midomo yake ilianza kubadilika rangi na kuwa ya bluu iliyokolea kabla ya kupoteza fahamu. Alikimbizwa hospitalini ambako madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake, lakini alifariki dunia siku mbili baada ya kula mlo huo.

Mkuu wa kijiji hicho, Laddy Gemang, alituma maofisa kuchunguza tukio hilo na walikuta magamba yenye rangi ang’avu ya kaa aina ya ‘devil crab’ kwenye taka za nyumbani kwake. Kaa hao wanajulikana kuwa na sumu kali ya neva (neurotoxins) inayoweza kusababisha kupooza na hata kifo.

Gemang alielezea kusikitishwa kwake na tukio hilo akisema: “Ni jambo la kuhuzunisha sana kwa sababu walipaswa kufahamu. Wanaishi karibu na bahari, wanajua kwamba ‘devil crab’ ni hatari kuliwa. Kwa nini basi akale?”

Emma Amit, aliyekuwa mvuvi mwenye uzoefu pamoja na mumewe, inaonekana alipuuzia hatari hiyo katika jitihada za kutengeneza maudhui yatakayovutia watazamaji wengi mtandaoni. Rafiki zake wameelezea kifo chake kuwa cha kushtua na cha ghafla.

Tukio hilo limeibua mjadala mkali mitandaoni, huku baadhi wakilaumu shinikizo la kutafuta umaarufu kupitia mitandao ya kijamii na wengine wakisema ni ajali inayotokana na hatari za mazingira.

Hili si tukio la kwanza la aina hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni, changamoto za kula kupita kiasi au vyakula hatarishi zimehusishwa na vifo vya watayarishaji wa maudhui.

Kifo cha Emma Amit kinaacha funzo kuhusu hatari za kuchukua maamuzi ya kuhatarisha afya kwa ajili ya maudhui ya mitandao ya kijamii.

Related Posts