
Kiongozi wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Said Issa Mohamed
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiongozi wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Said Issa Mohamed
Kiongozi wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Said Issa Mohamed, amesema yeye na wenzake waliamua kufungua shauri mahakamani kuhusu mgawanyo wa rasilimali za chama si kwa lengo la kukiua chama hicho, bali kuhakikisha kunakuwa na uwiano wa haki kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano.
Mohamed ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kufafanua hatua hiyo, baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, pamoja na Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi wa CHADEMA Zanzibar, Hamad Mussa Yussuf, kumshutumu kwa kudai anazungumza uongo.
Amesema wao hawakupeleka chama mahakamani kwa nia ya kukihukumu au kukivunja, bali kwa lengo la kukijenga na kukiimarisha ili kitende haki kwa pande zote mbili za Muungano.
“Nilisema sisi hatukuipeleka CHADEMA mahakamani kwenda kuihukumu katika misingi ya kuiua, bali kwa misingi ya kuijenga na kukiimarisha kuwa chama kitakachotenda haki kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano,” amesema Mohamed.
Mohamed, ambaye ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA Zanzibar, amesema anasikitishwa na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa chama yanayowataja wao kama mapandikizi au wasaliti wa chama, ilhali madai yao yalifikishwa kwanza ndani ya vikao halali vya chama.
Ameeleza kuwa malalamiko hayo yaliwasilishwa katika vikao vya Kamati Maalum ya CHADEMA Zanzibar na baadaye kupelekwa kwa uongozi wa chama kama maombi na mapendekezo, lakini hayakupata ufumbuzi.
Mohamed amesema katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, chama kimekuwa kikipewa ruzuku na Serikali, lakini Zanzibar imekuwa ikipata mgawo mdogo sana wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama.
Amefafanua kuwa mwaka 2025 chama kilikuwa kinapokea takribani Sh milioni 117 kwa mwezi, lakini Zanzibar ilipatiwa Sh milioni mbili pekee kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama.
Aidha, amesema kati ya mwaka 2015 hadi 2020 chama kilikuwa kinapokea zaidi ya Sh milioni 300 kwa mwezi, lakini mgawo wa Zanzibar uliendelea kubaki mdogo.
“Pamoja na hali hiyo tuliomba angalau asilimia 10 ya fedha hizo ziende Zanzibar ili kuendesha chama, haikuwezekana. Tukapendekeza hata asilimia tano, nako hakukukubaliwa,” amesema Mohamed.
Ameongeza kuwa kutokana na kushindikana kupata suluhu ndani ya vikao vya chama, waliamua kutafuta njia nyingine ya kisheria ambayo haitakidhuru chama.
Amesema kama wangeamua kupeleka suala hilo kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ingeweza kusababisha chama kufutwa, lakini hawakutaka kufikia hatua hiyo kwa sababu bado wanakipenda chama chao.
“Tungekwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, mambo yangekuwa tofauti na hata chama kingeweza kufutwa. Lakini sisi bado tunakipenda chama, ndiyo maana tumeenda mahakamani ili haki ya Zanzibar katika rasilimali za chama ipatikane,” amesema.
Mohamed pia amedai kuwa kwa sasa chama kimehama katika jengo la Makao Makuu madogo Zanzibar lililokuwa Mkwajuni kutokana na deni la Sh milioni 12.
Aidha, amesema licha ya chama kuwa na zaidi ya magari 20, Zanzibar haina hata gari moja la chama, jambo ambalo amesema limekuwa likilalamikiwa na viongozi wa Zanzibar tangu mwaka 2010.
Amesisitiza kuwa malalamiko hayo si mapya, kwani yamekuwa yakijadiliwa ndani ya vikao vya chama kwa muda mrefu, na kwamba lengo lao ni kuona kunakuwepo uwiano wa rasilimali unaowanufaisha wanachama wa pande zote za Muungano.
