
Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara, imeamuru kufungwa rasmi kwa Kampuni ya Sahara Media Group Limited baada ya kubainika kuwa imepatwa na mdororo mkubwa wa kifedha na kushindwa kujiendesha pamoja na kulipa madeni yake.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Dk. Mwajuma Kadilu kufuatia ombi la kampuni hiyo yenyewe kuomba kufilisiwa.
Ripoti zilizowasilishwa mahakamani na Afisa Mkuu wa kampuni hiyo, Steven Diallo, zimeonesha hali mbaya ya kifedha ya kampuni, ikiwemo kupata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 3.9 kwa mwaka 2023 pekee pamoja na mrundikano wa madeni ya kodi.
Imeelezwa kuwa kampuni hiyo ina deni la kodi la takribani Sh. milioni 97.7 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ushahidi wa kihasibu pia umeonesha kuwa takribani asilimia 80 ya mapato yote ya kampuni yalikuwa yakielekezwa katika kulipa madeni ya kodi, hali iliyosababisha kushindwa kuendesha shughuli za kila siku za vyombo vyake vya habari.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Kadilu amesema kuwa baada ya kuthibitika mwombaji anapata hasara kubwa na hana uwezo wa kulipa madeni yake, hatua sahihi ni kufungwa kwa kampuni hiyo.
Ili kuhakikisha mchakato wa kufungwa unafanyika kwa mujibu wa sheria, mahakama imewateua mawakili wasomi Alex Mgongolwa na Frank Mwalongo kuwa wasimamizi wa pamoja wa mchakato wa ufilisi kwa kipindi cha miezi mitatu.
Majukumu yao ni pamoja na kuchukua udhibiti wa mali zote za kampuni, kusimamia ulipaji wa madeni kwa wadai pamoja na kuzuia uhamishaji wowote wa mali au hisa kuanzia sasa
