Serikali Yaongeza Mabilioni Kuwainua Wabunifu Sekta ya Sanaa


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema serikali imeongeza zaidi ya Sh. bilioni 30, kati ya bilioni 20 zilizokuwa zimetengwa awali kwa ajili ya kuwawezesha vijana wanaojihusisha na sekta ya ubunifu nchini.

Walengwa wa mfuko huo, ni pamoja na watengeneza maudhui mtandaoni, wanamuziki, waigizaji, waandishi wa habari, watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii na wabunifu wa kazi mbalimbali za sanaa.

Akizungumza leo jijini Arusha, Waziri Makonda, amesema mfuko huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sekta ya habari, sanaa na ubunifu.

“Awali Wizara ilikuwa imepangiwa Sh. bilioni 20, lakini baada ya mazungumzo na Benki ya CRDB, kiwango hicho kimeongezwa na kufikia Sh. bilioni 50 ili kupanua wigo wa vijana watakaonufaika na mfuko huo,” amesema.
Pia Makonda, ameongeza kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni tarehe rasmi ya uzinduzi wa mfuko huo, na baada ya kuzinduliwa fedha zitaanza kutolewa kwa vijana wa sekta ya habari, sanaa na ubunifu ili kuwawezesha kukuza kazi zao na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa

Related Posts