CHADEMA Yaieleza UN Wasiwasi Kuhusu Mgogoro wa Kisiasa Tanzania

CHADEMA yaieleza UN wasiwasi kuhusu mgogoro wa kisiasa Tanzania
CHADEMA yaieleza UN wasiwasi kuhusu mgogoro wa kisiasa Tanzania

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewasilisha wasiwasi wake kwa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania, kufuatia mkutano kati ya ujumbe wa chama hicho na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa UN katika Umoja wa Afrika (AU), Parfait Onanga-Anyanga.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa Machi 12, 2026 na chama hicho ikielekezwa kwa Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, CHADEMA ilithibitisha kuwa mkutano huo ulifanyika Machi 10, 2026 jijini Dar es Salaam kama sehemu ya mashauriano yanayoendelea kuhusu mgogoro wa kisiasa Tanzania.

Ujumbe wa CHADEMA uliongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, ukiwa pia na Mwanasheria Mkuu wa chama, Rugemeleza Nshalla.

Katika mazungumzo hayo, chama hicho kilieleza kile kilichokiita wasiwasi mkubwa kuhusu ukandamizaji wa maandamano ya raia yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.

“CHADEMA imedai kuwa vikosi vya usalama vilitumia nguvu za mauti dhidi ya waandamanaji wasiokuwa na silaha waliokuwa wakipinga mchakato wa uchaguzi uliodaiwa kuwa umechezewa. Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na chama hicho, zaidi ya raia 2,000 walipoteza maisha huku maelfu wengine wakijeruhiwa,” imesema sehemu ya barua hiyo.
Chama hicho pia kilieleza kuwepo kwa madai ya kutisha yanayohusu juhudi za kuficha ukubwa wa mauaji hayo. Huku ripoti zikidai kuwa baadhi ya miili ya waathiriwa ilizikwa katika makaburi ya pamoja huku mingine ikidaiwa kuharibiwa katika michakato ya viwandani, ikiwemo ndani ya viwanda vya saruji.

Aidha, CHADEMA ilieleza wasiwasi wake kuhusu kuendelea kushikiliwa kwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Tundu Lissu, ambaye anazuiliwa katika Gereza la Ukonga kwa mashtaka ya uhaini ambayo chama hicho kinadai ni ya kisiasa.

Katika mazungumzo hayo, chama hicho pia kimeeleza kuwa kimekuwa kikishuhudia kudhoofika kwa uadilifu wa chaguzi nchini tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

CHADEMA imedai kuwa chaguzi zilizofanyika katika miaka ya karibuni, ikiwemo ya 2019, 2020, 2024 na 2025, hazikuwa na uwazi na uhalali.

Chama hicho kimeelekeza lawama kwa chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kikidai kuwa vinawajibika kwa matukio ya vurugu yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025.

Katika mkutano huo, CHADEMA imewasilisha mapendekezo kadhaa kwa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, yakiwemo kuachiwa huru kwa Tundu Lissu, kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya shughuli za chama hicho na kuanzishwa kwa tume huru ya kimataifa kuchunguza matukio ya vurugu yaliyotokea kati ya Oktoba na Novemba 2025.

Pia chama hicho kimeitaka jumuiya ya kimataifa kuanzisha uchunguzi huru kuhusu madai ya kutoweka kwa watu kwa nguvu pamoja na mauaji ya kiholela yanayodaiwa kutokea nchini tangu mwaka 2015.

CHADEMA pia imesema haitambui uhalali wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na imetoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi mpya chini ya mfumo ulioboreshwa wa kikatiba na kisheria wa uchaguzi.

Katika hitimisho lake, chama hicho kimesema kinaamini mgogoro wa kisiasa nchini unaweza kutatuliwa kwa njia ya amani na kidemokrasia kupitia mchakato unaojumuisha ukweli, uwajibikaji, maridhiano na mageuzi ya kisiasa.

Pia kimeeleza kuwa kiko tayari kushirikiana na utaratibu wowote wa kimataifa unaolenga kuhakikisha haki na uwajibikaji vinapatikana

Related Posts