
Taharuki imejitokeza katika barabara kuu ya Morogoro-Iringa majira ya saa nane usiku wa kuamkia Machi 19 mwaka huu baada ya Lori la mizigo kuonekana likiteketea kwa moto katika eneo la Lugono, Jirani kidogo na njia panda ya kuelekea Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia foleni ndogo ya magari yakisimama kupishana ili kulazimika kulikwepa Lori hilo lililokuwa limeshika moto mkubwa hasa maeneo ya mbele ya gari.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema moto huo ulianza ghafla na kusambaa kwa kasi, hali iliyosababisha uharibifu mkubwa wa sehemu ya mbele ya lori hilo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika eneo la tukio na kuudhibiti moto huo, na kuzuia usisambae zaidi maeneo mengine ama kuathiri watumiaji wengine wa barabara.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa mtu mmoja aliyekuwa ndani ya Lori anahofiwa kufariki dunia, ingawa bado jitihada kumpata Msemaji wa Jeshi la Polisi zinaendelea kubaini chanzo cha tukio hilo.
