Mmoja Afariki, Wawili Wajeruhiwa Wakibishania Simba na Yanga

Mmoja Afariki, Wawili Wajeruhiwa Wakibishania Simba na Yanga
Mmoja Afariki, Wawili Wajeruhiwa Wakibishania Simba na Yanga

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kutokea ugomvi uliotokana na ushabiki wa mpira kati ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga, katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amesema tayari wameanzisha msako wa kumtafuta kijana mmoja (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuua Abel Mganga Mazuri (25), mkazi wa Nyamahengo, na kuwajeruhi watu wengine wawili.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Machi 24, 2026, majira ya saa 5:30 usiku katika Kitongoji cha Nyamahengo, Kijiji na Kata ya Sumve, wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza msako wa kumtafuta kijana mmoja kwa tuhuma za mauaji ya Abel Mganga Mazuri (25), mkazi wa Nyamahengo, aliyeuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani. Mtuhumiwa pia aliwajeruhi watu wawili kwa kutumia kitu chenye ncha kali wakati wakinywa pombe na kuangalia mpira kwenye banda la maonyesho ya mpira katika Kata ya Sumve,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha shambulio hilo ni ushabiki wa mpira uliovuka mipaka na kusababisha ubishani mkali kati ya mashabiki wa klabu za Simba na Yanga.

“Waathirika wote wamepatiwa fomu za matibabu ya polisi (PF3) na hivi sasa wanapata matibabu katika Hospitali Teule ya Sumve ambapo hali zao zinaendelea kuimarika. Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtia mbaroni mtuhumiwa ili afikishwe katika vyombo vya sheria,” amehitimisha Kamanda Mutafungwa.

Related Posts