
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia Aprili 1, 2026 ambapo bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa petrol ni Tsh. 3820, dizeli Tsh.3806 na mafuta ya taa Tsh. 3684.
Taarifa ya EWURA imesema bei za mafuta katika soko la dunia zimeongezeka kwa asilimia 69.98 kwa mafuta ya petroli, asilimia 114.46 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 120.81 kwa mafuta ya taa ambapo mabadiliko ya bei za mafuta nchini kwa mwezi Aprili 2026 yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na vita inayoendelea kati ya Marekani kwa kushirikiana na Israeli dhidi ya Irani iliyoanza tarehe 28 Februari 2026.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa kushambuliwa kwa visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kusafisha mafuta (refineries) pamoja na Irani kufunga Lango la Hormuz linalopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa kwenda kwenye masoko mbalimbali duniani.
Hali hiyo imeathiri hali ya uzalishaji mafuta kwenye nchi za Mashariki ya Kati ambako Tanzania inaagiza kwa kiasi kikubwa; imeongeza gharama za usafirishaji kutokana na kukosekana kwa meli za kusafirisha mizigo na imeongeza gharama za bima za meli za mizigo kutokana na vita.
Ongezeko hilo la bei za mafuta ni janga la kidunia na Tanzania kama sehemu hiyo inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha usalama wa upatikanaji wa mafuta nchini na katika bei himilivu ili kupunguza madhara ya kiuchumi na kijamii. Kutokana na hali hiyo, wananchi wanashauriwa kutumia mafuta kwa uangalifu na ufanisi mkubwa,
Kwa mwezi Aprili 2026, gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 15.3 kwa mafuta ya petroli na asilimia 10.8 kwa mafuta ya dizeli na hakuna mabadiliko ya gharama kwa mafuta ya taa. Katika Bandari ya Tanga gharama zimeongezeka kwa asilimia 6.9 kwa mafuta ya petroli na hakuna mabadiliko kwenye mafuta ya dizeli. Hakuna mabadiliko ya gharama katika bandari ya Mtwara.
