
Tarehe rasmi za Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 zimethibitishwa, na hivyo kumaliza miezi kadhaa ya uvumi huku Afrika Mashariki ikiendelea na maandalizi yake.
Kenya, Uganda na Tanzania sasa zinaweza kuimarisha maandalizi yao ya kombe la Mataifa ya Afrika 2027 wakijua ni lini michuano hiyo itafanyika.
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe amesisitiza kuwa michuano hiyo haitasogezwa hadi 2028 au kuondolewa Afrika Mashariki na pia amethibitisha kuwa itafanyika kati ya Juni na Julai 2027.
Hata hivyo, hakukuwa na uthibitisho wa tarehe kamili, jambo ambalo sasa limekuwa wazi kufuatia taarifa ya Kamati ya maandalizi ya AFCON 2027 ya Uganda.
Wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, shirikisho la soka nchini Uganda AFCON 2027 lilithibitisha kuwa michuano hiyo itafanyika kuanzia Juni 19-Julai 18, 2027.
Kwa uthibitisho huo, nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kazi yake ni ngumu linapokuja suala la maandalizi kwani kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya ukaguzi wa CAF, ukanda huo bado upo nyuma ya ratiba ya viwanja na vifaa vya mazoezi vinavyohitajika kuandaa michuano hiyo.
