Chama cha Chadema Chaondolewa Katazo la Kufanya Siasa

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt, Rugemeleza Nshala, amesema Mahakama ya Rufaa imetoa uamuzi kwamba kuanzia leo April 15, 2026, hakuna zuio tena dhidi ya CHADEMA, hivyo Chama hicho kipo huru na Viongozi pamoja na Wanachama wake wanaruhusiwa kuendelea na shughuli za Siasa kama kawaida bila kuzuiwa na Polisi au mamlaka nyingine yoyote.

Akizungumza leo April 15, 2026, Makao Makuu ya Chama hicho Jijini Dar es salaam, Nshala amesema, “Asubuhi leo nikiwa sina hili wala lile nimepigiwa na Karani, nikamuuliza nani anasema, akasema naitwa Tina, una nini? Tuna uamuzi wa Mahakama tunatakiwa tukusomee ndani ya muda mfupi, nikawafahamisha Viongozi na Wanasheria wenzangu” amesema Dkt, Nshala.

Aidha ameendelea kwa kusema, “uamuzi ukasomwa, uamuzi umesema ile amri ya zuio ambayo ilitolewa na Jaji Mwanga ilikuwa batili, kwa kuwa baada ya Wakili Jebra Kambole kusema kwamba amejitoa kumwakilisha Katibu Mkuu na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, Mahakama haikutakiwa kuendelea kusikiliza ile kesi kwa sababu upande wetu Katibu Mkuu na Bodi ya Wadhamini hawakuwa Mahakamani, ili kuheshimu haki, ilitakiwa iwape nafasi ya kusikilizwa, hivyo zuio lile halipo”

Ameongeza kuwa, “Hata Polisi walikuwa wakilishadadia na kuwapiga wanawake wetu na Viongozi wa BAWACHA wakati wanaenda Musoma, lakini sasa amri hiyo haipo, nataka na Polisi wote mfahamu, Mahakama imesema hivi hakuna zuio lolote dhidi ya CHADEMA kuanzia leo Mtu asije akatokea Afande yoyote au nani akafanya hivyo, atakayefanya hivyo anakiuka amri ya Mahakama ya Rufaa, Chama hiki kipo huru kufanya kazi zake”

“Wanachama wote na Viongozi wote wa Chama chetu wana haki ya kufanya shughuli za Siasa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Dkt, Nshala.

Related Posts