
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa Mwanaharakati Hilda Newton kuwa Ijumaa ya April 24, 2026, kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai iliyopo katika Jengo la Makao Makuu Ndogo ya Polisi iliyopo Mtaa wa Ohio Jijini Dar es salaam ili kuwasilisha ushahidi wa taarifa aliyoitangaza kwa Umma kupitia mitandao ya kijamii kuwa Serikali imepanga kumuua Tundu Lissu kwa risasi.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Polisi hii leo April 22, 2026 imeeleza “Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kukusanya ushahidi kutokana na taarifa ya Hilda Newton aliyochapisha na kusambaza katika Mitandao ya Kijamii tarehe 10.4.2026 taarifa hiyo ilikuwa inasema pamoja na mambo mengine kuwa, Serikali imepanga kumuua Mhe. Lissu kwa risasi.”
“lli kukamilisha uchunguzi, Jeshi la Polisi linamwelekeza Hilda Newton afike katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai iliyopo katika Jengo la Makao Makuu Ndogo ya Polisi iliyopo Mtaa wa Ohio Jijini Dar es Salaam tarehe 24.4.2026 saa nne (4) asubuhi ili aweze kuwasilisha ushahidi aliyosema na kutangazia umma kuwa anao. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa yaJinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.”
