
Aliyekuwa Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Nigeria, Michael Eneramo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 40 baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mchezo wa kirafiki.
Kwa mujibu wa Shirikisho la soka nchini Nigeria (NFF), Eneramo alianguka dakika chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, ambapo inadaiwa alipata tatizo la moyo (cardiac arrest).
Mchezo huo ulifanyika eneo la Ungwan Yelwa, mjini Kaduna, na Eneramo alicheza kipindi chote cha kwanza kabla ya tukio hilo kutokea.
Katibu Mkuu wa NFF, Mohammed Sanusi, alisema ameshtushwa na msiba huo akieleza kuwa ni pigo kubwa kwa soka la Nigeria.
Eneramo aliichezea Nigeria mara 10 baada ya kufanya maamuzi ya kukataa kuchezea Tunisia, ambako alicheza soka la kulipwa kwa mafanikio makubwa. Alijulikana zaidi akiwa na klabu ya Espérance Sportive de Tunis ambapo alishinda mataji mbalimbali.
Katika maisha yake ya soka la klabu, pia aliwahi kucheza Uturuki kwenye timu za Sivasspor, Beşiktaş na İstanbul Başakşehir.
Eneramo alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa kwa Nigeria mwaka 2009 dhidi ya Jamaica, na akafunga bao lake la kwanza dhidi ya Ireland miezi michache baadaye.
