
Shirikisho la Soka Ulimwenguni, FIFA limetupilia mbali pendekezo la Italia kuchukua nafasi ya Iran kwenye michuano ya Kombe la Dunia la 2026 baada ya wazo hilo kutolewa na mjumbe maalum wa Marekani, Paolo Zampolli aliyependekeza Italia kupewa nafasi hiyo kutokana na mzozo unaoendelea kati ya Iran, Marekani na Israel.
Aidha Waziri wa michezo wa Italia, Andrea Abodi na Waziri wa Uchumi, Giancarlo Giorgetti wamekataa pendekezo hilo wakisisitiza kwamba kufuzu kwa Italia kushiriki Kombe la Dunia kunapaswa kupatikane uwanjani na sio kupitia njia nyingine.
Hata hivyo FIFA haijatoa maoni yake ya moja kwa moja kuhusu pendekezo hilo, lakini imeonyesha kuwa hakuna msingi wa wa kubadilisha timu ambazo zimefuzu huku Rais wake, Gianni Infantino akisisitiza kuwa timu ya Taifa ya Iran itashiriki michuano hiyo bila mashaka yoyote.
Italia ambao ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia la FIFA hawatashriki michuano hiyo kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kupoteza mechi yao ya mchujo wa kufuzu World Cup 2026 (WC2026) dhidi ya Bosnia & Herzegovina mwezi uliopita.
