
Da es Salaam. Mfanyabiashara Fred Ngajiro maarufu kama Fred Vunjabei, aliyeongoza kura za maoni ndani ya Jimbo la Isimani kwa kupata kura 2,703, amewekwa kando katika uteuzi wa mwisho wa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mdogo wa jimbo hilo.
Badala yake, CCM imemteua Emmanuela Mtatifikolo ambaye katika kura za maoni alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 621.
Uamuzi huo umebainishwa leo Aprili 29, 2026 katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia mamlaka ya Kamati Kuu chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 (Toleo la Julai 2025).
“Kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la Julai 2025, Kamati Kuu imefanya uteuzi wa mgombea wa CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Isimani, lililopo Wilaya ya Iringa Vijijini. Mgombea aliyeteuliwa ni Emmanuela Kaganda Mtatifikolo,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika matokeo ya kura za maoni yaliyoshirikisha wagombea 18, Vunjabei aliongoza akifuatiwa na Festo Kiswaga aliyepata kura 873, huku Mtatifikolo akishika nafasi ya tatu.
Mtatifikolo kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Babati kabla ya kuhamishwa kutoka Arumeru.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Isimani unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi, kilichotokea Machi 25, 2026
Mwananchi
