Mwamba Aliyemuua EX Wake na Kumtupa Ununio Ahukumiwa Kunyongwa

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es salaam imemhukumu kunyongwa hadi kufa (death by hanging) Abdalah Mussa maarufu Mr. Bluu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi aliyekuwa mpenzi wake, Ezenia Kamana.

Hukumu hiyo imesomwa leo na Jaji Awamu Mbagwa kufuatia ushahidi wa Mashahidi 25 wa upande wa mashtaka, vielelezo 15 pamoja na utetezi wa Mshtakiwa, ambapo Mahakama ilieleza ushahidi uliowasilishwa umejitosheleza kuthibitisha bila kuacha shaka la msingi kuwa Mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa makusudi. akisoma hukumu hiyo Jaji Mbagwa amesema, “ushahidi uliopo unajitosheleza kuwa Mshtakiwa alimuua Ezenia kwa makusudi na mashtaka yamethibitishwa bila kuacha shaka la msingi dhidi yake, Abdalah Mussa Miraji ninakutia hatiani kwa kosa la kumuua Ezenia Kamana kwa makusudi, hata hivyo, kama upande wowote hauridhiki, una haki ya kukata rufaa,” alisema Jaji Mbagwa.

Aidha, mahakama ikieleza tukio hilo lilitokea Agosti 19, 2024 eneo la Chang’ombe Wilaya ya Temeke baada ya ugomvi unaodaiwa kuchochewa na madai ya Sh100,000 kutoka kwa marehemu, Mahakama ilibaini baada ya tukio Mshtakiwa hakuchukua hatua za kuokoa maisha ya marehemu, badala yake aliondoka na mwili huo hadi Nyumbani kwake na kuutekelezea vitendo vya kuficha ushahidi, huku ushahidi ukidai mwili wa marehemu ulikatwa vipande na kusambazwa katika maeneo ya Ununio, Tegeta na Kunduchi, Mahakama pia ilieleza wawili hao walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa takribani miaka minne kabla ya tukio hilo.

Katika hatua nyingine, imeelezwa wakati jitihada za kumtafuta marehemu zikiendelea Mshtakiwa alikuwa hapokei simu hali iliyozua mashaka yaliyochochea uchunguzi uliomfikisha Mahakamani, huku hukumu hiyo ikihitimisha kesi hiyo kwa Mahakama kusisitiza kuwa pande zote zina haki ya kukata rufaa iwapo hazitaridhika na maamuzi hayo.

Related Posts