Mwamba Akataa Wito wa Kuliwakilisha Taifa Lake Kombe la Dunia

Wakati wanasoka wengi wakitamani kuwakilisha timu zao za Taifa kwenye michuano mbalimbali ya Kimataifa huku wengine wakilazimika kubadili timu za Taifa na kuwakilisha Nchi nyingine kama taratibu zinaruhusu, hali imekuwa tofauti kwa nyota wa klabu ya RC Lens ya Ufaransa, Odsonne Edouard.

Mshambuliaji huyo raia wa Ufaransa
amezua gumzo baada ya kukataa nafasi ya kuiwakilisha Nchi ya Haiti kwenye mashindano ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuitwa kwani wazazi wake wana asili ya Nchi hiyo iliyopo Kaskazini mwa Amerika ambayo imefuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974.

Akielezea uamuzi huo, nyota huyo aliyeifungia Lens mabao 14 kwenye michezo 36 kwenye michuano yote msimu huu likiwemo bao pekee kwenye fainali ya Kombe la Ufaransa dhidi ya OGC Nice, amesema hajihisi kuwa na uhalali wa kucheza Kombe la Dunia kwa sababu kuna wachezaji walioipigania Nchi kufuzu na yeye hakuhusika.

“Simi sipo tayari kuja dakika za mwisho na kunufaika na juhudi zao. Kwa kifupi, kama nitacheza, basi ni lazima nistahili.” — amesema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 akiamini itakuwa si haki kwa wachezaji waliopigana katika kampeni nzima ya kufuzu ili kupata nafasi ya kihistoria.

Haiti ambayo ipo Kundi C kwenye michuano ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 itaanza kampeni zake dhidi ya Scotland Juni 14, 2026 kabla ya kuivaa Brazil Juni 20 2026 na kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya Waafrika, Morocco Juni 25, 2026.

Related Posts