
Fiorentina Yataka Kumsajili Kinara wa Mabao AFCON U-17 Dismas Athanasi
Klabau ya Fiorentina ya nchini Italia imeendelea kufuatilia kwa karibu nyota chipukizi wa Tanzania, Dismas Shida Athanasi, ambaye ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji waliovutia zaidi katika michuano ya AFCON U17 iliyofanyika nchini Morocco.
Athanasi, alimaliza mashindano hayo akiwa mfungaji bora kwa kufunga mabao matatu na kutwaa tuzo ya Golden Boot baada ya kuiongoza Serengeti Boys kufika fainali ya AFCON U17 kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.
Taarifa kutoka barani Ulaya zinaeleza kuwa Athanasi Ameanza kuvutia macho ya maskauti kutoka klabu kadhaa za Ulaya, huku Fiorentina ikitajwa kuwa miongoni mwa timu zinazofuatilia maendeleo yake kwa karibu.
kijana huyo amesifiwa kwa uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti za ushambuliaji, utulivu akiwa mbele ya lango na uwezo mkubwa wa kusoma mchezo licha ya umri wake mdogo. Wataalamu wengi wa soka la vijana wanaamini kuwa anaweza kuwa mmoja wa nyota wakubwa wa Tanzania katika miaka ijayo endapo ataendelea kupata mazingira bora ya maendeleo.
Athanasi ambaye ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa katika safu ya ushambuliaji, alitajwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika AFCON U17 ya mwaka 2026, jambo lililofanya mafanikio yake kuwa ya kipekee zaidi. Licha ya ushindani mkubwa kutoka kwa washambuliaji wa mataifa mbalimbali, aliweza kuongoza orodha ya wafungaji na kuipa Tanzania heshima kubwa kwenye soka la vijana barani Afrika.
Iwapo Fiorentina itaamua kuchukua hatua rasmi za kumsajili siku zijazo, Athanasi anaweza kuwa mmoja wa wachezaji wachache kutoka Tanzania kuingia katika mfumo wa maendeleo wa klabu kubwa za Serie A. Kwa sasa, macho ya wengi yanaendelea kumtazama kijana huyo ambaye tayari ameanza kuandika historia yake katika soka la Afrika akiwa bado na umri mdogo sana.
Follow @shabbygraphicx
