
Askofu wa Kanisa Katoliki Auawa Kwa Kupigwa Risasi Msumbiji
Askofu wa Kanisa Katoliki, Osorio Citora Afonso, aliyeteuliwa kuhudumu katika Jimbo la Quelimane katikati mwa Msumbiji, ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa Nyumbani kwake katika mazingira ambayo bado hayajafafanuliwa.
Kwa mujibu wa Msemaji wa ofisi ya uchunguzi wa uhalifu, Maximino Amilcar, Askofu huyo mwenye umri wa miaka 54 alipigwa risasi kifuani, katika makazi yake yaliyoko Quelimane.
Maafisa wa uchunguzi wameeleza tukio hilo kama mauaji ya kutumia silaha za moto, huku wakisema bado ni mapema kutoa maelezo kamili kuhusu chanzo cha uhalifu huo.
Katika taarifa yake, Mkutano wa Maaskofu wa Msumbiji ulisema kuwa Afonso alipatikana amefariki katika mazingira ya kutatanisha yanayohitaji uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa kilichotokea.
Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, alieleza masikitiko yake makubwa kufuatia kifo hicho, akisema taifa limepoteza Kiongozi muhimu wa kidini na kwamba ni hasara kubwa kwa jamii ya Msumbiji.
Mamlaka za Msumbiji zimeanzisha uchunguzi ili kubaini waliohusika na sababu za mauaji hayo.
