Mtanzania Barka Seif Mpanda Aweka Historia, Asajiliwa Akademi ya Barcelona La Masia

Mtanzania Barka Seif Mpanda Aweka Historia, Asajiliwa Akademi ya Barcelona La Masia
Mtanzania Barka Seif Mpanda Aweka Historia, Asajiliwa Akademi ya Barcelona La Masia

Kinda wa Kitanzania, Barka Seif Mpanda, ameandika historia mpya katika soka la Tanzania baada ya kuwa Mtanzania wa kwanza kusajiliwa katika Akademi maarufu ya Barcelona, La Masia, akitokea akademi ya CF Damm nchini Hispania.

Hatua hiyo kubwa imekuja baada ya Barka kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika mashindano mbalimbali ya vijana, ambapo alifanikiwa kufunga mabao 41 katika michezo 28 pekee. Takwimu hizo zimevutia viongozi wa La Masia ambao waliamua kumpa nafasi ya kujiunga na moja ya akademi zinazoheshimika zaidi duniani katika kuzalisha vipaji vya soka.

La Masia imekuwa chimbuko la baadhi ya nyota wakubwa waliowahi kutamba katika soka la dunia, wakiwemo Lionel Messi, Xavi Hernández, Andrés Iniesta na wengine wengi waliopitia mfumo huo kabla ya kufikia mafanikio makubwa katika soka la kimataifa.

Kupitia ujumbe wake baada ya kuthibitishwa kujiunga na La Masia, Barka alieleza furaha yake na kusema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa ndoto alizokuwa nazo tangu akiwa mdogo.

“Ndoto zangu zimetimia kujiunga na La Masia. Naushukuru uongozi wa CF Damm kwa kunisaidia katika misimu mitatu niliyokuwa nao. Nawashukuru makocha, wachezaji wenzangu na familia kwa kufanikisha jambo hili,” alisema Barka.

Katika kipindi chake akiwa CF Damm, Barka alionyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kuwa miongoni mwa wachezaji waliotegemewa zaidi katika kikosi hicho. Mafanikio yake yamekuwa yakifuatiliwa kwa karibu na wataalamu wa soka nchini Hispania, jambo lililopelekea kupata nafasi ya kuhamia Barcelona.

Usajili wa Barka unaonekana kuwa habari njema kwa soka la Tanzania kwani unafungua mlango kwa vijana wengine wenye vipaji kuamini kuwa wanaweza kufikia viwango vya juu zaidi vya soka duniani kupitia nidhamu, juhudi na kujituma.

Wadau mbalimbali wa michezo nchini Tanzania wamepokea kwa furaha taarifa hizo, wakieleza kuwa mafanikio ya Barka ni ishara ya maendeleo ya vipaji vya Kitanzania katika anga la kimataifa. Wengi wameeleza matumaini kuwa kijana huyo ataendelea kufanya vizuri na siku moja kuwakilisha Tanzania katika ngazi za juu za soka duniani.

Kwa sasa, macho ya mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania na Hispania yataelekezwa kwa Barka Seif Mpanda kuona namna atakavyoendelea kuimarika katika mazingira mapya ya La Masia, akademi ambayo imezalisha baadhi ya mastaa wakubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya mchezo wa soka.

Ikiwa ataendelea na kiwango chake bora, Barka ana nafasi kubwa ya kuandika historia nyingine zaidi katika maisha yake ya soka na kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi kipya cha wachezaji wa Tanzania wanaotamani kucheza katika vilabu vikubwa vya Ulaya.

Related Posts