Waziri wa Nishati “Bei ya Mafuta Kushuka Julai”

Waziri wa Nishati "Bei ya Mafuta Kushuka Julai"
Waziri wa Nishati “Bei ya Mafuta Kushuka Julai”

Waziri wa Nishati, Wizara ya Nishati Tanzania Deogratius Ndejembi, amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba bei ya mafuta Nchini Tanzania itashuka kuanzia mwezi Julai 2026 kufuatia kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Akijibu swali kuhusu upatikanaji wa nishati hiyo leo Juni 26, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, Waziri Ndejembi amesema mabadiliko hayo yamechangiwa na utulivu wa hali ya usambazaji wa mafuta duniani pamoja na mazungumzo ya amani yanayoendelea katika maeneo muhimu ya usafirishaji wa nishati.

Ameeleza kuwa Serikali imezielekeza Taasisi muhimu za sekta ya mafuta, zikiwemo TPDC, EWURA pamoja na mamlaka nyingine za bandari na usambazaji, kuhakikisha kuwa punguzo lolote la bei ya dunia linawafikia moja kwa moja Wananchi.

“Tumewataka EWURA kuhakikisha Mtanzania anaanza kuona nafuu ya bei ya mafuta kuanzia mwezi ujao,” amesema Waziri Ndejembi.

Ameongeza kuwa kuna meli kadhaa za mafuta ambazo tayari ziko njiani na nyingine zipo bandarini pamoja na kwenye ghala (storage), hali inayotarajiwa kusaidia kuongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo Nchini.

Kwa mujibu wa Serikali, ndani ya wiki nane hadi kumi zijazo, masoko ya dunia yanatarajiwa kurejea kwenye viwango vya mwanzo wa mwaka 2026, hatua ambayo inaweza kuleta utulivu zaidi wa bei ya nishati Nchini.

Related Posts