
Simba SC Yatoa Kauli Nzito: Usajili Bado Mtamu, Hakuna Anayeondoka, Simba Day Kupigwa Uwanja wa Uhuru!
Uongozi wa Simba SC umewatoa hofu mashabiki wake na kuwatahadharisha kukaa mkao wa kula kuelekea msimu mpya wa 2026/27, ukisisitiza kuwa zoezi la usajili bado linaendelea moto mtupu.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya klabu hiyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameeleza kuwa kikosi kipo kwenye hatua za mwisho za kuelekea Rwanda kushiriki Michuano ya CECAFA Kagame Cup—ambayo itatumika kama sehemu ya maandalizi ya msimu (pre-season).
Ahmed Ally amebainisha kuwa, ingawa wameshatambulisha baadhi ya ingizo jipya, bado kuna vyuma vingine vinakuja:
“Usajili wetu bado haujafungwa. Leo tuliamua kupumzika kidogo ili kutoa nafasi kwa matangazo yaliyopita kueleweka vizuri, lakini kuanzia kesho tutaendelea na utambulisho wa wachezaji wengine wapya.”
Ukweli Kuhusu Wachezaji Wanaotajwa Kuondoka
Kuhusu tetesi za kuondoka kwa nyota kama Libasse Gueye, Anicet Oura, Inno Loemba, na Selemani Mwalimu, Ahmed amezikanusha vikali taarifa hizo na kuweka wazi kuwa wote bado ni wachezaji halali wa Simba SC. Amesisitiza kuwa klabu haitaendeshwa kwa shinikizo la mitandao ya kijamii, bali itafanya maamuzi kwa maslahi ya timu na kutoa taarifa rasmi.
Simba Day 2026 Kutimkia Uwanja wa Uhuru
Pia, Ahmed Ally ametangaza rasmi kuwa Tamasha la Simba Day 2026 litafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kutokana na Uwanja wa Benjamin Mkapa kuendelea kufanyiwa matengenezo. Tamasha la mwaka huu litakuwa la kipekee kwani litaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, ambapo mashabiki watapata fursa ya kukishuhudia kikosi kamili cha msimu wa 2026/27.
