
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya hofu iliyotolewa na shirika la World Liberty Congress linalotetea Demokrasia, Haki za binadamu, utawala wa Sheria, na uhuru wa kisiasa duniani, kuhusu usalama wa Mwenyekiti, Mhe. Tundu Lissu, ambaye hadi sasa bado anaendelea kuwa kizuizini.
Kwa mujibu wa taarifa ya leo Julai 27, 2026 iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA , Brenda Rupia, Chama hicho kimemtaka Mkuu wa Gereza la Ukonga kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuhakikisha usalama wa Mwenyekiti Tundu Lissu, na kutoa taarifa kuhusu hali yake, pamoja na kuhakikisha kwamba haki zake za kikatiba na za kibinadamu zinaheshimiwa kikamilifu.
CHADEMA imesema imepata hofu na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa kiongozi huyo, na hali yake kwa ujumla akiwa chini ya uangalizi wa dola kwa zaidi ya siku 472 ikiwa ni baada ya miaka ya mateso ya kisiasa ikiwemo kunusurika katika jaribio la mauaji, kukamatwa kamatwa, na kukabiliwa na mashtaka yanayoonekana kuwa na msukumo wa kisiasa kutokana na msimamo wake thabiti wa kutetea demokrasia, haki za binadamu, Reforms za Katiba, na utawala wa sheria.
CHADEMA imesema Jeshi la Magereza lina wajibu wa kikatiba na kisheria kulinda kila mtanzania na kusisitiza kuwa halitakubaliana na madhara yoyote au tishio la usalama wa Mwenyekiti Lissu akiwa kizuizini huku ikiendelea kutoa wito wake wa kutaka aachiwe huru mara moja bila masharti maana Lissu sio mhaini na hana hatia yoyote.
“Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, taasisi za kidemokrasia, na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya Mwenyekiti Lissu na kutumia njia zote za kidiplomasia na kisheria zilizopo kudai kuheshimiwa kwa haki zake.” imesema sehemu ya taarifa ya Chama hicho kikuu cha upinzani Nchini.
Kitenge
