
Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umetangaza Jumatatu kuwa unapanga kufuta visa za muda mfupi (non-immigrant visas) za raia wa Kigeni ambao wameomba hifadhi nchini Marekani au wanaendelea kutafuta hadhi ya hifadhi, ikiwa ni hatua nyingine katika kampeni kubwa ya serikali hiyo ya kukabiliana na Uhamiaji.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema wizara hiyo inashirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa (DHS) “kuwatambua na kuwafutia visa wageni walioingia nchini Marekani wakidai kuwa ni wageni wa muda mfupi, lakini baadaye wakaomba hifadhi ili kubaki nchini humo kwa kudumu.”
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje haikueleza idadi kamili ya visa vinavyotarajiwa kufutwa katika mpango huo.
Kwa mujibu wa ripoti, idadi ya wageni ambao visa zao za biashara na utalii zinapangwa kufutwa inaweza kufikia 200,000. Ikiwa mpango huo utatekelezwa kwa kiwango hicho, unaweza kuwa kufutwa kwa visa kwa watu wengi zaidi kwa wakati mmoja katika historia ya Marekani.
Nyaraka za Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na maafisa wawili wa Marekani ikisema kuwa serikali inapanga kufuta visa za aina ya B1 na B2 zilizotolewa kati ya mwaka 2016 na 2026 kwa watu ambao wamewahi kuomba hifadhi au ambao kwa sasa wanaendelea na maombi ya hifadhi.
Visa za B1 na B2 hutolewa kwa watu wanaosafiri kwenda Marekani kwa shughuli za biashara au utalii.
Hata hivyo, kufutwa kwa visa hivyo hakumaanishi moja kwa moja kwamba wahusika watafukuzwa mara moja nchini humo. Kwa mujibu wa AP, watu wengi ambao kesi zao za hifadhi bado zinaendelea wanaweza kubadilishiwa hadhi yao ya uhamiaji, lakini watapoteza hadhi yao ya kuwa wageni wa biashara au watalii.
