
Mwigizaji Mkongwe wa NIGERIA Pete Edochie Afariki Dunia
Mwanga wa tasnia ya filamu nchini Nigeria umezimika kufuatia kifo cha mwigizaji mkongwe na maarufu, Pete Edochie, aliyefariki dunia Jumatano, Novemba 25, 2026, akiwa na umri wa miaka 79.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia yake kupitia mwanawe, Leo Pete Edochie, mwigizaji huyo alifariki saa 12:30 alfajiri katika jimbo la Enugu, Nigeria, baada ya kuugua saratani ya tezi dume kwa muda mrefu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa familia imepokea msiba huo kwa huzuni kubwa, huku mipango ya mazishi ikitarajiwa kutangazwa baadaye.
Pete Edochie alikuwa miongoni mwa waigizaji wenye majina makubwa katika tasnia ya filamu ya Nigeria, maarufu kama Nollywood.
Alijipatia umaarufu mkubwa kupitia uigizaji wake wa mhusika Okonkwo katika filamu ya televisheni Things Fall Apart ya mwaka 1987, iliyotokana na riwaya maarufu ya mwandishi wa Nigeria, Chinua Achebe.
Uigizaji wake katika kazi hiyo ulimjengea heshima kubwa na kumfanya atambulike ndani na nje ya Nigeria.
Kabla ya kuingia katika tasnia ya filamu, Pete Edochie alikuwa mtangazaji wa redio. Alianza kazi yake mwaka 1967 katika Shirika la Utangazaji la Nigeria Mashariki (Eastern Nigerian Broadcasting Corporation), ambako alipanda ngazi mbalimbali hadi kushika nyadhifa za uongozi katika katika Shirika la Utangazaji la Anambra (Anambra Broadcasting Service).
Katika safari yake ya uigizaji, alishiriki katika filamu nyingi zilizopata umaarufu, zikiwemo Rituals, Billionaire’s Club na Lionheart ya mwaka 2018, ambamo aliigiza kama Chief Ernest Obiagu.
Mchango wake katika filamu, televisheni na utangazaji umeacha alama kubwa katika tasnia ya burudani barani Afrika. Atakumbukwa kwa sauti yake nzito, busara, matumizi ya methali za Kiafrika na uwezo wake wa kuigiza wahusika wenye mamlaka na hekima.
