
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Chimaguli Majiyangui Samamba (54) Mkulima na Mkazi wa Ugede_Songambele kwa tuhuma za kumuua mke wake kwa sababu ya kuchelewa kurudi nyumbani.
Taarifa ya leo Oktoba 9, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi imeeleza kuwa mnamo Oktoba 8, 2025 majira ya saa 12:00 jioni katika Kitongoji cha Ugede, kata ya Salawe, Tarafa ya Nindo Wilaya na Mkoa wa Shinyanga Moshi Paulo John, (47), Mkulima na Mkazi wa Ugede-Songambele aligundulika kuuawa na mwili wake kufukiwa kwenye shimo lililopo jirani na nyumbani kwake.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mnamo Oktoba 1, 2025 majira ya saa 4:00 usiku marehemu Moshi akiwa nyumbani kwake aligombana na mume wake Samamba, ugomvi uliotokana na kuchelewa kurudi nyumbani kwa marehemu kwani usiku huo alirudi nyumbani toka matembezini na kumkuta mumewe nyumbani.
Samamba alimshambulia marehemu kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hadi mke wake kuishiwa nguvu na kufariki dunia na baada kubaini kuwa mkewe amefariki dunia alichukua mwili wa marehemu na kwenda kuutupa nje pembeni mwa nyumba yao kwenye shimo lililokuwa likichimbwa kwa matumizi ya choo na aliweza kuufukia mwili huo kwa udongo.
Baada ya marehemu kutokuonekana kwa kipindi chote tangu Oktoba 2, 2025, majirani walianza walianza kupata wasiwasi na pia kutokana na mazoea ya mume kumpiga mkewe mara kwa mara hivyo mnamo oktoba 7, 2025 taarifa zilifikishwa kwa mwenyekiti wa kitongoji ambaye alifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumhoji lakini alikana kuhusika na uhalifu wowote dhidi ya mkewe.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mnamo Oktoba 8, 2025 majira ya saa 5:00 asubuhi mwenyekiti alitoa taarifa kituo kidogo cha Polisi Salawe na kwa haraka zaidi Polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumkamata na baada ya mahojiano ya awali mtuhumiwa alikiri kumuua mkewe na kumfukia kwenye shimo la choo lililopo nyumbani kwake.

