
Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga amefariki akiwa na umri wa miaka 80.
Raila amefariki wakati akifanyiwa matibabu katika hospitali moja nchini India kulingana.
Rais wa Kenya William Ruto ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni, Rais Ruto alimtaja Odinga kama “mzalendo mwenye ujasiri usio wa kawaida.”
Alisema bendera ya taifa itapepea nusu mlingoti kote nchini Kenya na katika balozi zote za Kenya nje ya nchi.
“Kama ishara ya heshima, nimeahirisha shughuli zangu zote za umma kwa siku zijazo, na ninawaomba wafanyikazi wengine wote wa umma na viongozi kufanya vivyo hivyo ili tujiunge na taifa katika kipindi hiki cha maombolezo,” Ruto alisema.
Rais Ruto pia ametangaza kuwa Odinga ataandaliwa mazishi ya kitaifa kwa heshima kamili.
Aliongeza kuwa serikali ya India, ambapo waziri mkuu huyo wa zamani alifariki alipokuwa akipokea matibabu, imejitolea kuwezesha kurejeshwa kwa mwili wake.
Ujumbe unaoongozwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi na mnjane wa Odinga Mama Ida Odinga, unatarajiwa kusafiri kuelekea India kusimamia mipango hiyo.
Kumekuwa na uvumi kuhusu afya ya kiongozi huyo wa ODM katika wiki za hivi majuzi baada ya kutoweka kwenye hafla za umma mwezi uliopita.
Kakake mkubwa, Seneta wa Siaya Oburu Oginga, Jumamosi alisema alikuwa mgonjwa lakini “anapata nafuu n kupumzika” nchini India, na hakuwa katika hali mbaya kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa kwenye vyombo vya habari.
Odinga ambaye amemwacha mjane na watoto watatu ni mwanasiasa mashauhuri wa Kenya ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kuanzia 2008 hadi 2013.
Kabla ya kifo chake kiongozi huyo atakumbukwa kwa kupigania uhuru wa kidemokrasia, haki za kibinadamu na mabadiliko ya kitaifa.
Safari yake ya kisiasa
Raila Odinga alikuwa mtu mashuhuri katika siasa za Kenya na Afrika, na kutia moyo kizazi chote barani.
Akiwa mwana wa mpiganiaji uhuru Jaramogi Oginga Odinga, makamu wa kwanza wa rais wa Kenya, Raila alisomea Ujerumani Mashariki kabla ya kurejea nyumbani miaka ya sabini.
Aliwekwa kizuizini kwa miaka sita baada ya kutuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi mwaka 1982, na baadaye alikamatwa tena kwa kushinikiza demokrasia chini ya utawala wa chama kimoja.
Alirejea kutoka uhamishoni baada ya kuanzishwa tena kwa siasa za vyama vingi kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge. Alikuwa na mchango mkubwa katika kukomesha utawala wa miongo kadhaa wa chama cha uhuru wa Kenya alipounga mkono jitihada za Mwai Kibaki za kuwania urais mwaka 2002.
Raila Odinga ambaye anajulikana sana kama Baba, aligombea urais mara tano, mara nyingi akiunganisha na kuunda upya upinzani, lakini hakuwahi kunyakua wadhifa huo wa juu zaidi.
Vita vyake vikali vilikuja kati ya mwaka 2007, wakati matokeo ya uchaguzi yaliogombaniwa kuzua ghasia nchi nzima, hatua iliosababisha makubaliano ya kugawana madaraka yaliyosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.
Safari ndefu ya kisiasa ya Raila Odinga, iliyojaa ukakamavu, ukaidi na kujitolea mhanga, ilimletea sifa ndani na nje ya nchi.

