
Dar es Salaam. Benchi la Ufundi la Taifa Stars leo Machi 18, 2026 limetangaza kikosi cha wachezaji 25 kitakachoshiriki mashindano ya FIFA Series 2026 huko Rwanda huku likiwaacha wachezaji 11 ambao walikuwemo katika kikosi kilichoshiriki Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2025.
Baadhi ya wachezaji hao wameachwa kwa sababu ni majeruhi huku wengine wakiwekwa kando kutokana na sababu za kiufundi.
Katika kikosi kilichotangazwa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi leo, wachezaji waliokuwemo katika kikosi cha AFCON 2025 ambao hawajajumuishwa ni Hussein Masalanga, Yakoub Mohamed, Shomari Kapombe, Mbwana Samatta, Lusajo Mwaikenda, Dickson Job, Wilson Nangu, Kibu Denis, Abdul Selemani ‘Sopu’, Pascal Msindo na Habib Idd ‘Gego’.
Job, Nangu, Gego na Sopu kwa sasa ni majeruhi na waliobakia hawajajumuishwa kwa sababu za kiufundi na kocha Gamondi.
Kuna urejeo wa kipa Aishi Manula na kiungo Mudathir Yahya ambao hawakupata fursa ya kuitwa katika kikosi kilichoishia hatua ya 16 bora ya fainali za AFCON 2025.
Kocha Gamondi amewapa fursa wachezaji Mohamed Mussa wa Mashujaa FC na Bakari Msimu kuingia kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Taifa Stars.
Kipa Yona Amosi wa Pamba Jiji FC amejumuishwa pia kikosini kama ilivyo kwa mshambuliaji nyota wa JKT Tanzania, Paul Peter.
Wachezaji 25 wanaounda kikosi cha Taifa Stars kitakachoshiriki FIFA Series na klabu zao kwenye mabano ni Aishi Manula, Zuberi Foba, Twalib Nuru, Elias Lameck, Feisal Salum na Iddi Suleiman (Azam FC), Bakari Mwamnyeto, Mohamed Hussein, Ibrahim Abdulla na Mudathir Yahya (Yanga), Nickson Kibabage, Yusuph Kagoma na Suleiman Mwalimu (Simba), Yona Amosi na Kelvin Nashoni (Pamba Jiji).
Wengine ni Mohamed Mussa (Mashujaa FC), Bakari Msimu (Coastal Union), Haji Mnoga (Salford City), Novatus Dismas (Goztepe), Alphonce Mabula (Shamakh), Saimon Msuva (Al Talaba), Kelvin John (Aalborg), Charles M’mombwa (Floriana), Tarryn Allarakhia (Rochdale) na Paul Peter (JKT Tanzania).
