Mwanachama hai na shabiki kindakindaki wa klabu ya Yanga Sc Haji Sunday Manara ameibuka na hoja nzito mara baada ya klabu hiyo kulalamika kwamba mpaka sasa bado hawajalipwa pesa zao za ubingwa wa CRDB Federation Cup ambazo walishinda msimu uliopita mara baada ya kuwa mabingwa wa michuano hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa na klabu ya Yanga Sc siku ya leo Jumatatu tarehe 9 Juni, inaeleza kwamba TFF ambao ndio wasimamizi wakuu wa michuano hiyo mpaka sasa bado hawajawalipa Yanga Sc pesa hizo kitu ambacho kimepelekea viongozi wa klabu hiyo kufanya maamuzi magumu ya kugomea mechi ijayo ya fainali kama watakuwa hawajalipwa pesa hizo.

Mara baada ya klabu ya Yanga Sc kutoa taarifa hiyo kwa umma, Haji Manara amekuja na hoja mpya kabisa ambapo ameeleza wazi kwamba mtu pekee aliyekwamisha mchakato wa Yanga Sc kulipwa pesa mpaka sasa ni Rais wa TFF Wallaca Karia.

Manara anaamini kwamba benki ya CRDB haiwezi kulimbikiza deni la klabu ya Yanga Sc bali inawezekana kwamba walishawalipa TFF na pesa hizo kwa sasa zitakuwa zimekwamia kwenye mikono ya Wallace Karia pamoja na viongozi wake wengine.

Manara katika taarifa yake amefika mbali zaidi kwa kueleza kwamba Karia pia anapaswa kuachia ngazi kwenye shirikisho hili kwa sababu ameshindwa kuwajibika vyema ikiwa ni pamoja na kufanya janja janja kwenye pesa ambazo Yanga Sc walipaswa kulipwa tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Haji Sunday Manara kwa kiasi kikubwa amekuwa na changamoto zake na kiongozi huyu, wanapokuwa yanatokea madhaifu kama haya basi huwa anajiinua na kumshambulia kwa maneno makali kitu ambacho hakina busara wala faida kwenye mpira wetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *