Historia Yaandikwa: Kiswahili Chapitishwa Kuwa Lugha Rasmi ya CAF

 

Historia Yaandikwa: Kiswahili Chapitishwa Kuwa Lugha Rasmi ya CAF
Historia Yaandikwa: Kiswahili Chapitishwa Kuwa Lugha Rasmi ya CAF

 

Historia Yaandikwa: Kiswahili Chapitishwa Kuwa Lugha Rasmi ya CAF

Abuja, Nigeria – Lugha ya Kiswahili imeidhinishwa rasmi kuwa mojawapo ya lugha za mawasiliano za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kufuatia marekebisho ya Katiba ya shirikisho hilo yaliyopitishwa jijini Abuja, Nigeria.

Uamuzi huo wa kihistoria umetangazwa na Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, mara baada ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 48 wa CAF kupiga kura nyingi za kuunga mkono pendekezo hilo.

Lugha Rasmi za CAF Zafikia Tano

Kwa hatua hii mpya, Kiswahili kinaungana na lugha nyingine nne ambazo zimekuwa zikitumika kikatiba, na kufanya jumla ya lugha rasmi za CAF kufikia tano:

  • Kiswahili

  • Kiingereza

  • Kifaransa

  • Kiarabu

  • Kireno

Lugha hizi sasa zitatumika rasmi katika nyaraka, mikutano, mawasiliano, pamoja na matukio yote makubwa yanayoandaliwa na kusimamiwa na shirikisho hilo barani Afrika.

Pongezi kwa Mataifa ya Afrika Mashariki

Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, amezipongeza nchi za Tanzania, Kenya, na Uganda kwa jitihada na mchango wao mkubwa uliowezesha Kiswahili kupata hadhi hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo ni fursa muhimu ya kuunganisha Waafrika kupitia michezo.

Kauli ya Serikali ya Tanzania

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa—ambaye alimwakilisha Waziri Paul Makonda katika mkutano huo—amesema Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki zimeupokea uamuzi huo kwa heshima na fahari kubwa.

Akiwa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Selestine Kakele, pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, Msigwa ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia na kuunga mkono mchakato wa kuiomba CAF kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi tangu ulipoanzishwa miaka mitatu iliyopita.

Msigwa amesisitiza kuwa Tanzania itatumia fursa hiyo kikamilifu kukuza Kiswahili na utamaduni wa Mswahili katika majukwaa ya kimataifa, huku ikifungua milango ya ajira na ushiriki mpana zaidi kwa wataalamu wa lugha hiyo katika tasnia ya michezo barani Afrika.

Related Posts