
Meneja wa zamani wa Chelsea na Manchester United, Mbwatukaji Jose Mourinho ameripotiwa kuwa ukingoni kuteuliwa kuwa kocha mkuu mpya wa klabu ya Real Madrid baada ya vigogo hao wa Uhispania kukumbwa na mwenendo usioridhisha tangu kuondoka kwa Carlo Ancelotti.
Real Madrid ambayo imeshindwa kutwaa ubingwa wa Laliga kwa msimu wa pili mfululizo ilimteua Xavi Alonso kuchukua mikoba ya Carlo Ancelotti mnamo Juni 2025 kabla ya kumtimua miezi 7 baadaye huku nafasi yake ikichukuliwa na Alvaro Arbeloa ambaye pia ameshindwa kufikia matarajio ya mabosi wa klabu hiyo.
Mourinho ambaye aliinoa Real Madrid kati ya mwaka 2010 na 2013 yupo mstari wa mbele kwenye orodha ya makocha wanaopigiwa upatu kuchukua mikoba ya Arbeloa huku klabu hiyo ikimuona Mreno huyo kama mtu sahihi wa kuleta sauti ya mamlaka ndani ya kikosi hicho baada ya ripoti za msuguano baina ya wachezaji klabuni hapo.
Hata hivyo hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Real Madrid na kocha huyo wa sasa wa Benfica lakini ripoti zinaeleza kwamba mazungumzo ya awali yameanza kati ya wakala wa Mourinho, Jorge Mendes na uongozi wa Mabingwa hao mara 15 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
