
Umewahi kusikia baadhi ya watu ambao walikuwa na tabia hatarishi zilizowafanya wakakutana na watu mbalimbali, hata wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), lakini walipopimwa hawakubainika? Wanasayansi wanatoa jawabu; watu hao wana ulemavu katika vinasaba vyao kwa kukosa vipokezi au vikombe sahani vijulikanavyo kama CXCR4 na CCR5.
Akizungumza Daktari aliyefanya tafiti kadhaa zihusuzo kirusi cha Ukimwi, Lilian Mwakyosi, amesema hitilafu hiyo huwasaidia kirusi hicho kushindwa kuingia katika DNA zao na mwishowe huondoka mwilini kama takamwili nyingine zinavyotoka.
Amesema VVU vinahitaji njia mbili za kuingia ili kupenya mwilini, na ikiwa njia moja imezibwa, virusi haviwezi kupenya. “Katika maisha ya kibinadamu kuna watu ambao wana hitilafu ya kinasaba, ambayo katika seli zao hizi nyeupe, hawana hivi vipokezi vyenye uwezo wa kuruhusu kirusi cha Ukimwi kuingia katika seli hizi hai nyeupe. Hivyo mtu huyu hawezi kupata maambukizi ya VVU,” amesema.
Dk Mwakyosi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, amesema watu hao ni wachache sana na hakuna kwa sasa vipimo hapa nchini vinavyomsaidia mtu huyu kujua kama yeye ni miongoni mwa watu hao.
Pamoja na kundi hilo, amelitaja kundi la pili kuwa ni baadhi ya watu pale maambukizi yanapotokea, huwa wanakuwa katika hali tofauti za kinga, miili yao huwa na mapokeo tofauti kutokana na sababu mbalimbali za vinasaba.
Kuna baadhi ya watu wachache pia wameonekana na hali fulani, ambapo wanaweza kupata VVU lakini mwili wao una uwezo wa kudhibiti VVU visizaliane; vikabaki katika kiwango cha chini na haviongezeki. “Ndiyo maana kuna watu unaweza kukutana naye akakwambia aligundua ana maambukizi mwaka 1997 na alikaa miaka mitatu, 10 na zaidi bila kutumia ARV.
“Hata hivyo, haimaanishi kwamba mtu huyu asitumie ARV. Ni muhimu kutumia ili asiendelee kuwaambukiza wengine, pia kinga inaweza kushuka na kumletea madhara,” amesema. Kwa mujibu wa Dk Mwakyosi, watu hawa wamekuwa wakitumika zaidi katika kutafuta chanjo na tiba ya VVU.
“Wao, kirusi kikiingia mwilini na kuathiri seli, seli inatuma taarifa kuwa kuna shida, halafu mwili unatengeneza kinga tunaziita antibodies. Wale ambao wanapata maambukizi na kuna hitilafu nyingine huku zinazuia shambulio zaidi la seli zao, hao ndiyo watakuwa na antibodies na ndiyo ambao wamekuwa wakitumika zaidi kwenye upande wa kupata tiba na chanjo,” amesema.
Jinsi maambukizi yanavyotokea. Dk Mwakyosi ameeleza kwa kina namna kirusi cha Ukimwi kinavyoingia mwilini na kujizalisha, huku akifafanua kuwa huenda kujishikiza kwenye DNA na hiyo imesababisha ugumu katika kupata tiba yake. Amesema kirusi kinapoingia mwilini mwa binadamu, huenda kujishikiza katika seli nyeupe za damu na ambazo huwa zinaathiriwa zaidi ni seli hai aina ya CD4, ukiacha nyingine nyingi tofauti.
