
Sardar Azmoun, Mmoja wa Wachezaji mashuhuri wa Kandanda wa Iran, amefukuzwa katika timu ya Taifa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokuwa mwaminifu kwa Serikali na hivyo kufanya kusiwe na uwezekano wa kushiriki katika Michuano ya Kombe la Dunia.
Ushiriki wa Iran katika kombe la Dunia kwa ujumla uko chini ya wingu kwa sababu ya mzozo unaoendelea na Marekani, ambao ni waandalizi wa Mashindano ya Juni 11-Julai 19 wakiwa na Mexico na Canada.
Iwapo timu ya Taifa itashiriki katika mechi zao za mwanzo za makundi, bila shaka itadhoofika kwa kukosekana kwa mshambuliaji Azmoun, ambaye amefunga mabao 57 katika mechi 91 za Kimataifa tangu alipoanza kucheza mwaka 2014 akiwa kijana.
Azmoun, ambaye anacheza soka katika timu ya Shabab Al-Ahli iliyopo Umoja wa Falme za Kiarabu, alizisikitisha mamlaka za Iran wiki hii kwa kutuma picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa na mtawala wa Dubai Mohammed bin Rashid Al Maktoum.
Iran imefanya mashambulizi ya roketi na ndege zisizo na rubani katika UAE kufuatia mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel, ambayo yalimuua Kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei.
