Mwabukusi: Sigombei Ubunge, Mapambano Yataendelea UraianiMwabukusi: Sigombei Ubunge, Mapambano Yataendelea Uraiani

Mwabukusi: Sigombei Ubunge, Mapambano Yataendelea Uraiani

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika TLS, Boniface Mwabukusi amebainisha kuwa kupigania utawala wa sheria, haki za binadamu na ulinzi wa rasilimali za asili za Tanganyika kunaweza kufanyika Vyema zaidi akiwa nje ya Bunge la Tanzania, hivyo hajadhamiria na hafikirii kuwania nafasi ya Ubunge wa Tanzania.

Kupitia Chapisho lake alilochapisha kwenye Mtandao wake wa X, Mwabukusi ameeleza kuwa amelazimika kuyaandika hayo kufuatia kile alichobainisha kuwa amekuwa akiulizwa maswali mengi na baadhi ya watu ikiwa atagombea nafasi ya Ubunge ama nafasi yoyote ya kuchaguliwa katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu. Katika andiko lake Mwabukusi ameeleza;

“Kipaumbele changu cha kwanza kwasasa ni kupigania utawala wa sheria ,haki za binadamu na ulinzi wa Raslimali za Asili za Tanganyika.

2.Kipaumbele changu cha pili nikutaka na kuhakikisha uwajibikaji kwa kuhakikisha wale wote waliopotezwa wanarejeshwa na walio umizwa wafidiwe na Serikali iwawajibishe wahusika wote.Hatutakiwi kunyamaza au kunyamazishwa.Tutatumia vyombo vya ndani na nje kuhakikisha haki kwa ndugu zetu.

3.Nitapambana kujenga Uzalendo wa kweli wa Taifa.Uzalendo ni kupinga uzembe katika utumisho wa umma, dhuluma ,wizi,ukatili,utekaji na uonevu.

4.Nataka kukamilisha mchakato wa kusikilizwa kwa rufaa yetu dhidi ya DPW kuhusu mkataba wa Bandari kwani hatutakubali raslimali muhimu za Tanganyika kuwa katika mikono ya wageni kwa mkataba wa namna hii.Ni laana.

5.Nitakuwa na jukumu kubwa la kuishawishi na kuitaka serikali kuwrka wazi mikataba yote inayohusu Raslimali Asili za Tanganyika ili watanganyika tuione ,tuijadili na kuridhia iwapo imekidhi vigezo na kuzingatia maslahi ya Tanganyika.

6.Kufanyia kazi na kushiriki na wananchi wazawa wa maeneo ya pembezoni kuhusu haki yao ya kumiliki ardhi na ulinzi wahaki hiyo dhidi ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Hivyo kwa kuzingatia vipaumbele hivi na zaidi kwamba vinaweza kufanyika vyema nisipokuwa mbunge na kwa maslahi ya Tanganyika ninashawishika kutogombea nafasi yeyote ya kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2025.” Amesema Mwabukusi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *