Sheikh Alhad Mussa: Wanaomuandama Rais Samia Wapate Kiharusi na Stroke
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na amani nchini Tanzania JMAT, Sheikh Alhad Mussa Salum amewakosoa wale wote wanaomuombea na kumtabiria mabaya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema wote wanaomsemea na kumtabiria mabaya Rais Samia wapate magonjwa ya kiharusi na “stroke”.
“Yeyote atakayemtakia mabaya mama huyu, Mwenyenzi Mungu ampe stroke ya hatari, semeni Amen…. yeyote atakayemuandama mama huyu na kumtakia shari, Mwenyenzi Mungu ampe kiharusi kikubwa sana, semeni Amen…. Hii Amen yenu haitapotea, utapata stroke, utapata kiharusi na utakaa chini ili watanzania waendelee kupokea maendeleo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.”Amesema Sheikh Alhad.
Sheikh Alhad amebainisha hayo wakati wa uzinduzi wa soko jipya la nyama choma la Kumbilamoto Vingunguti Jijini Dar Es salaam akiambatana na Viongozi mbalimbali wa Jumuiya hiyo, akieleza kuwa Viongozi wa dini ni miongoni mwa mashuhuda wa kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia kote nchini Tanzania kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Kiongozi Mkuu wa nchi.
Aidha Sheikh Alhad amesisitiza kuwa zipo na anazisikia baadhi ya chokochoko zinazoendelea nchini, akibainisha pia kuona majaribio kadhaa ya kumkwamisha Rais Samia, akisisitiza kuwa chokochoko hizo zitashindwa na zitalegea kama ambavyo yamekuwepo majaribio mengi huko nyuma na ambayo yalifeli mapema.