
MJUMBE wa Tume ya Uchunguzi wa ghasia wakati na baada ya uchaguzi, Prof. Ibrahim Juma, amesema katiba inasema wazi kwamba kila mtu anahaki ya kuwa na maoni na kwamba kuna watu ambao ndio wanataka maoni yao yasikike na hiyo inaonekana zaidi kwenye mitandao ya kijamii.
Amesema mtu akijitokeza na kutoa maoni yake anashambuliwa kama nyuki akidhani kuwa hiyo sio afya katika hatua ambayo wanakwenda “tunataka tuwe na soko la mawazo kila mmoja anatoa mawazo, na mawazo yanashindana, lakini hii tabia ya kuzima mawazo ya wengine sio sawa.”
“Sisi wengine baada ya taarifa kutoka tumepokea simu za matusi zaidi ya 300 kwasababu kuna mtu hataki maoni yetu yaliyopatikana kwa njia ya methodolojia ambayo tumeonyesha yasijulikane kwa Watanzania, nadhani hilo ni jambo la hatari sana.
“Unaposema wewe ni muumini wa demokrasia wa haki za binadamu kuwa tayari kusikiliza maoni na mawazo ambayo wewe hupendi kuyasikiliza,” amesema Prof. Juma, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 28, 2026, mkoani Dar es Salaam.
Kadhalika, Prof. Juma ameeleza kuwa Mahakama Kuu iliwapa uhalali kisheria wa kuwapo na kufanya kazi, na kwamba uhalali wa Tume hiyo ulithibitishwa na Mhakama Kuu ya Tanzania.
“Wengi wamekuwa wakihoji uhalali wa tume yetu. Nataka kuweka rekodi sawa. Mahakama Kuu ya Tanzania, katika Shauri Namba 12 la Mwaka 2025, ilitoa uamuzi wa wazi kuwa Rais ana mamlaka kikatiba kuunda tume za uchunguzi, na kwamba Tume hii imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32,” amesema Prof. Juma.
Amesema uamuzi huo ulitolewa baada ya baadhi ya watu kufungua kesi mahakamani kupinga uwepo wa Tume. “Jaji amesema wazi: Tume hii ni halali. Kazi zake ni halali. Ushahidi uliokusanywa ni halali.”
Prof. Juma ameeleza kuwa kinga hiyo ya kisheria ndiyo iliyoiwezesha Tume kuwaita na kuwahoji wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa mikoa, makamanda wa polisi, viongozi wa vyama vya siasa, na wananchi wapatao 63,603 bila woga.
“Tusingeweza kukamilisha kazi hii kama tusingekuwa na ngao ya kisheria kutoka Mhimili wa Mahakama,” amesisitiza.
“Uhalali wa ripoti hii haukutoka Ikulu pekee ulithibitishwa na Mahakama. Kilichobaki sasa ni Watanzania kuisoma, kuijadili, na taasisi husika kuchukua hatua stahiki,” amethibitisha Prof. Juma.
