Uhaba ng’ombe wapandisha bei ya nyama, sasa kilo 20,000/-

Uhaba ng’ombe wapandisha bei ya nyama, sasa kilo 20,000/-
Uhaba ng’ombe wapandisha bei ya nyama, sasa kilo 20,000/-

Serikali ya Zanzibar imeeleza kuwa ongezeko la bei ya nyama linaloshuhudiwa visiwani humo kutoka wastani wa Sh. 14,000 hadi kufikia Sh. 20,000 linatokana na uhaba wa ng’ombe katika soko la ndani pamoja na ushindani mkubwa wa ununuzi wa mifugo kutoka Tanzania Bara unaofanywa na nchi jirani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk. Soud Hemed, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Chukwani.

Dk. Soud amesema Zanzibar inategemea zaidi ya asilimia 90 ya ng’ombe wanaotoka Tanzania Bara ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani. Hata hivyo, ongezeko la mahitaji ya mifugo kutoka nchi za Comoro, Kenya na Uganda limeongeza ushindani wa ununuzi, hali inayosababisha kupanda kwa bei za ng’ombe na hatimaye kuathiri bei ya nyama kwa walaji.

Amesema ng’ombe ambaye hapo awali alinunuliwa kwa wastani wa Sh700,000 sasa huuzwa kwa hadi Sh1.2 milioni, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa bei ya nyama katika soko la Zanzibar.

Kwa upande mwingine, Serikali imeanza kutekeleza hatua mbalimbali za kupunguza gharama za biashara ya mifugo ili kudhibiti ongezeko la bei ya nyama. Miongoni mwa hatua hizo ni kupunguza ada ya kibali cha usafirishaji wa mifugo kutoka Sh30,000 hadi Sh2,500.

Kwa mujibu wa Dk. Soud, hatua hiyo inalenga kurahisisha biashara ya mifugo, kuongeza upatikanaji wa ng’ombe sokoni na kusaidia kushusha bei ya nyama kwa manufaa ya wananchi.

Related Posts