Dk. Nchimbi mgeni rasmi Siku ya Mazingira Duniani

Dk. Nchimbi mgeni rasmi Siku ya Mazingira Duniani
Dk. Nchimbi mgeni rasmi Siku ya Mazingira Duniani

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani (WED) 2026 yatakayofanyika Juni 5, 2026 katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma, akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. ‎

‎Taarifa hiyo imetolewa Juni 4, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, wakati alipotembelea mabanda ya maonesho kuelekea kilele cha maadhimisho hayo.

‎Akizungumza katika ziara hiyo, Masauni ametoa wito kwa sekta zote nchini kuongeza juhudi za utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanafikiwa kwa ufanisi.

‎Amesema utunzaji wa mazingira ni ajenda ya kitaifa inayohitaji ushiriki wa kila sekta ya uchumi na si jukumu la wizara au taasisi moja pekee, akibainisha kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira salama na yanayohifadhiwa ipasavyo.

‎Kwa mujibu wa Masauni, sekta za mawasiliano, usafiri, kilimo, mifugo na uvuvi zinapaswa kuzingatia kanuni na miongozo ya uhifadhi wa mazingira katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku ili kupunguza athari zinazoweza kuhatarisha ustawi wa mazingira.

‎Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka msisitizo mkubwa katika usimamizi wa mazingira na kuongeza uwezo wa taifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo ushiriki wa sekta zote ni muhimu.

‎“Mazingira ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, lazima kila sekta ihakikishe inachangia katika uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira,” amesema Masauni.

‎Aidha, amewahamasisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kilele cha maadhimisho hayo, akisema ni fursa muhimu ya kujifunza, kuelimishana na kujadili mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za mazingira.

‎Maadhimisho ya mwaka huu yamewakutanisha taasisi za umma na binafsi, wadau wa mazingira pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi

Related Posts