Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) ya takwimu za afya duniani iliyochapishwa ikionesha athari kubwa zaidi za kiafya zilizosababishwa na janga la COVID-19 kuhusu vifo, muda wa kuishi na hali ya afya na ustawi kwa ujumla, imeweka wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili pekee, kati ya mwaka 2019 na 2021, matarajio ya kuishi yalipungua kwa mwaka mmoja na miezi minane ikiwa ni maporomoko makubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni hali iliyobatilisha mafanikio ya afya yaliyopatikana kwa muongo mmoja.
Haidong Wang, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu na Uchambuzi ya Shirika la afya duniani akiwa katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, Uswisi anaeleza moja ya taarifa ya kushangaza inayopatikana katika ripoti hiyo.
“Mojawapo ya matokeo muhimu ni kwamba magonjwa yasiyo ya kuambukiza sasa yanachangia zaidi ya nusu ya vifo katika makundi ya umri chini ya miaka 70. Ingawa idadi ya vifo vimepungua katika kundi hilo la umri, idadi ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza imeongezeka.”
Vyanzo vya tatizo viko katika mitindo ya maisha. Haidong Wang anaeleza,
“Matumizi ya tumbaku ni mojawapo ya sababu kuu za mwenendo huu. Ingawa matumizi ya pombe yamepungua katika maeneo mengi, katika maeneo mengine hali imekwama bila maendeleo zaidi. Udhibiti wa shinikizo la damu na kisukari bado haujafikia viwango vya kuridhisha, na uchafuzi wa hewa unaendelea kuathiri afya ya watu duniani kote.”
Hata hivyo moja ya taarifa nzuri katika ripoti hiyo inasema viwango vya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) na Kifua Kikuu vinaendelea kupungua, na idadi ya watu wanaohitaji matibabu kwa magonjwa ya tropiki yaliyopuuzwa imepungua lakini taarifa mbaya ni kuwa ugonjwa wa malaria umeanza kuongezeka tena tangu mwaka 2015, na usugu wa vijiumbemaradhi dhidi ya dawa bado ni changamoto kubwa kwa afya ya umma
ALSO READ | Mfalme Zumaridi Aachiwa Kwa Dhamana